Mfuko wa SELF ulio chini ya Wizara ya Fedha umefanikiwa kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa Shilingi bilioni 196.9 kuanzia 2021 hadi Juni 30, 2025 ili kuwawezesha wajasiriliamali na taasisi mbalimbali nchini Tanzania kupata mikopo kwa urahisi.
Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa mfuko wa SELF, Bi. Santiel Yona, tarehe 15/08/2025 wakati akitoa hotuba yake kwenye mkutano na waandishi wa habari na wahariri uliofanyika katika ukumbi wa King Jada Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa mikopo hiyo imewafikia wanufaika 1,83381; kati yao wanawake wakiwa 97,000 na wanaume wakiwa 86,000 na taasi 549 za kifedha.
Aidha Bi. Santiel amesema mfuko huo umefanikiwa kutengeneza ajira 183,000 kwa Watanzania, kutoa mikopo kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na kutoa elimu ya fedha mara kwa mara kupitia makongamano, maonesho kama Nanenane na vyombo vya habari.
Kulingana na hotuba yake Mfuko wa SELF umekutana na changamoto mbalimbali kama vile wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kifedha, wakopaji kutorejesha mikopo kwa hiari na wananchi wengi kujishughulisha na biashara zisizo rasmi.
Pia Bi. Santiel ameongeza kuwa taasisi imeweka mipango mikakati ya kuwa na wanufaika 200,000 kwa kipindi cha miaka mitano (2025- 2030) kwa kutoa mikopo ya kiasi cha Shilingi bilioni 300, kutoa elimu ya mikopo, kuongeza matawi kutoka 12 hadi 22 kufikia 2030, kuongeza ufanisi kwa kutoa huduma bora zaidi kwa teknolojia na uendelevu wa taasisi.