Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limemuua msemaji wa kundi la Hamas, Abu Obeida, katika shambulio la anga lililofanywa Jumamosi kwenye mji wa Gaza, taarifa ambayo hadi sasa haijathibitishwa na Hamas.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, aliipongeza IDF na Shirika la Usalama wa Ndani la Israel (Shin Bet) kwa kile alichokiita "utekelezaji sahihi" wa mauaji hayo, akionya kwamba kampeni dhidi ya washirika wa Hamas itaendelea.
“Wengi zaidi walioshirikiana na Obeida katika uhalifu watalengwa katika kampeni inayoendelea huko Gaza,” aliandika Katz kupitia mtandao wa X.
Hata hivyo Hamas bado haijatoa tamko la moja kwa moja kuthibitisha kifo cha msemaji huyo. Badala yake, kundi hilo liliripoti kuwa makumi ya raia waliuawa na kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel katika jengo la makazi lililopo katika kitongoji cha al-Rimal, mji wa Gaza.
Kwa mujibu wa waandishi wa habari waliopo eneo hilo, takribani watu saba waliuawa na zaidi ya 20 kujeruhiwa katika shambulio hilo, wakiwemo watoto.
Shambulio hilo limefanyika wakati mashambulizi ya anga ya Israel yakiongezeka mjini Gaza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kile kinachotajwa na Israel kama operesheni kubwa ya kutwaa udhibiti wa jiji la Gaza.
IDF na Shin Bet wamesema shambulio la Jumamosi lilikuwa mahsusi kwa lengo la kumuua Abu Obeida, wakieleza kuwa lilitokana na ufuatiliaji wa muda mrefu wa kijasusi.