Wananchi watitosha ujenzi wa eneo la uwanja wa ndege licha ya zuio

Wananchi Kata ya Shibula Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza walioko kwenye mgogoro wa ardhi kati yao na uwanja wa ndege wameazimia kuanza kuyaendeleza maeneo yao ikiwa ni pamoja na kujenga makazi kuanzia Oktoba mwaka huu endapo Serikali haitashughulikia mgogoro huo.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la kufanyia mikutano katika eneo hilo wananchi hao wamedai wamefikia maamuzi hayo baada ya kuchoshwa na kusubiri ahadi zisizotekelezeka kutoka Serikalini kwa takribani miaka 9 huku wakiwa wamezuiwa kuendeleza maeneo kwa ahadi ya kulipwa fidia ili kupisha uwanja wa ndege.

Kwa mujibu wa wananchi, mgogoro huo ulianza baada ya eneo hilo kutengwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege hatua iliyosababisha kusitishwa kwa uendelezaji wa makazi hayo.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Mgogoro wa Ardhi Kata ya Shibula, Robert Luzili ameunga mkono uamuzi huo akibainisha kuwa baadhi ya wakazi wamepewa uthamini wa mali kupitia hati zisizo na vielelezo halali zenye namba kutoka 1 hadi 96, zinazowatambua kama wamiliki wa maeneo hayo.

Akitoa ufafanuzi juu ya mgogoro huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewataka wananchi hao kuacha kujichukulia sheria kwani suala hilo limefikishwa kwenye mamlaka husika za ngazi za juu za Serikali na linaendelewa kufanyiwa kazi pindi mwarobaini ukipatikana wataletewa majibu.

"Kauli ya Bunge ilikuwa ni kuwataka wale watu waondoke tena bila fidia lakini tulipo zungumza na Waziri Mkuu, aliita mawaziri wenye dhamana kulitafakari jambo hilo vizuri na alitoa maelekezo kwamba wananchi hao kwa sasa wasibughudhiwe, wasiondolewe wakati Serikali inatafuta njia sahihi ya kumaliza suala hilo," amesema.

Mtanda ameongeza kuwa "Tunasubiri Serikali ichakate itakapofikia hatima yake tutaletewa taarifa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa na sisi tunao wajibu wa kuwaeleza nini kinachoendelea,".

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii