Wahamiaji watano waliofukuzwa Marekani na kutumwa Ghana wachukuwa hatua za kisheria

Wakati Rais wa Ghana John Dramani Mahama akithibitisha kuwasili katika nchi yake wahamiaji 14 wa Afrika Magharibi waliofukuzwa kutoka Marekani kufuatia makubaliano kati ya Accra na Washington, watano kati yao wameamua kupinga haraka uhalali wa uhamisho wao kwenda Ghana katika mahakama za Marekani.


Nchini Ghana, utata mpya umeibuka kufuatia kutangazwa kwa makubaliano kati ya Washington na Accra, ambapo nchi hiyo ya Afrika Magharibi inajiunga na orodha ya nchi zilizokubali kuwapokea wahamiaji haramu waliofukuzwa kutoka Marekani, ambazo ni RwandaEswatini na Sudan Kusini.

Wakati Rais wa Ghana John Dramani Mahama alithibitisha Jumatano, Septemba 10, kwamba kundi la raia 14 wa Afrika Magharibi waliwasili Ghana na watasafirishwa katika nchi zao za asili, watano kati yao wamefungua kesi kwa dharura nchini Marekani kupinga uhalali wa kufukuzwa kwao.

Je, uamuzi wa Ghana kukubali raia wa Afrika Magharibi waliofukuzwa kutoka Marekani utakuwa kinyume na katiba ya Ghana? Hii, angalau, ndivyo upinzani wa bunge la Ghana unadai. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa, Septemba 12, wanachama wa New Patriotic Party walionyesha kuwa hakuna makubaliano kama hayo ambayo yamewasilishwa Bungeni ili kuidhinishwa, ingawa katiba inatoa masharti hayo.

Hofu ya "kujifungamanisha" na sera ya Trump

Hofu nyingine iliyoibuliwa na wabunge wa upinzani: kwamba Ghana ingetoa "hisia ya kujipatanisha na serikali ya sasa ya Marekani inayodhibiti uhamiaji, inayokosolewa kwa ukali na ubaguzi wake." Madai haya yalijibiwa Septemba 15 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana mwenyewe, Samuel Okudzeto Ablakwa.

"Rais tayari ametangaza kwamba kundi la kwanza la watu waliofukuzwa, 14 kwa idadi, tayari wamewasili Accra. Miongoni mwao ni raia wa Nigeria na Gambia, ambao walisaidiwa kurejea katika nchi zao. Rais hana chochote cha kuficha juu ya suala hili. Mkataba huu wa Makubaliano na Marekani ulijadiliwa kwa kina na Ofisi ya rais, na pia uliandaliwa kwa ushauri wa Mkataba Mkuu. haujapelekwa Bungeni kwa ajili ya kuridhiwa." Ghana haijapokea wala kutaka kupata fidia yoyote ya kifedha au manufaa ya uwezo kuhusiana na Mkataba huu wa Maelewano.

Uamuzi wetu unakusudiwa tu kutoa kimbilio la muda inapohitajika, kuzuia kuteseka zaidi kwa wanadamu, na kudumisha uaminifu wetu kama mhusika anayewajibika katika kanda. Haipaswi kutafsiriwa kama kuunga mkono sera za uhamiaji zinazoedeshwa na utawala wa Donald Trump.

Mawakili wa wahamiaji hao wanaamini kuwa makubaliano haya yanaweza kuweka maisha yao hatarini. Kundi la walalamikaji linaundwa na Wanigeria watatu na Wagambia wawili ambao walichukuliwa kutoka kizuizini huo Louisiana mnamo Septemba 5 kabla ya kupakiwa kwa nguvu kwenye ndege ya kijeshi ya Marekani bila kujulishwa wanakoenda, kulingana na malalamiko yaliyowasilishwa kwa niaba yao. Kulingana na waraka huo, baadhi yao wanadaiwa kuzuiliwa kwa zaidi ya saa 16 na kwa sasa wanazuiliwa nchini Ghana katika mazingira ya "kinyama".

Uhamisho wa "udanganyifu"

Kati ya watu hao watano, mmoja—mwanamume mwenye jinsia mbili—tayari amerejeshwa nchini Gambia, nchi yake ya asili, ambako analazimika kujificha, kwani ushoga unachukuliwa kuwa ni kosa la jinai mjini Banjul.

Akielezea uhamishaji huu kama "udanganyifu" kwa sababu unaweza "kukwepa" taratibu za ulinzi wa mahakama zinazotolewa kwa baadhi ya wahamiaji, jaji anayesikiliza kesi hata hivyo anajiona kuwa hana uwezo wa kutaka walalamikaji warudi Marekani.

Hata hivyo, jaji huyo amewataka wawakilishi wa serikali ya Marekani kutoa taarifa ya kiapo ya hatua ilizochukua ili kuhakikisha kuwa wahamiaji hao hawatarejeshwa katika nchi ambako kuna uwezekano wa kuteswa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii