Nchini Kenya, mahakama imetoa siku ya Jumanne kibali cha kukamatwa kwa mwanajeshi wa Uingereza. Mwanajeshi huyo anashukiwa kumuua Agnes Wanjiru, mama mwenye umri wa miaka 21 ambaye mwili wake ulipatikana kwenye tanki la maji taka la hoteli ya Nanyuki mnamo mwaka 2012.
"Tunafurahia sana maendeleo haya, ingawa mfumo wa haki nchini Kenya umesubiri kwa muda mrefu," anaeleza Esther Njoki, mpwa wa Agnes Wanjiru. Ilichukua miaka 13 kwa jaji kuona kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuhalalisha hati ya kukamatwa.
Leo, askari wa Uingereza anatafutwa na mahakama. Ilikuwa ni pamoja na mwanajeshi huyu ambapo Agnes Wanjiru alionekana mara ya mwisho karibu na mji huu katikati mwa nchi, ambapo kunapatikana kitengo cha mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya, Batuk.
Hati hii ya kukamatwa inawakilisha hatua muhimu mbele kwa familia yake. Hata hivyo, Mbiyu Kamau, wakili wa familia ya Agnes Wanjiru, bado yuko makini. "Hatukufahamishwa hata kuwa kibali hiki kimetolewa. Ukosefu huu wa uwazi unatutia wasiwasi. Kesi hii iliingiliwa na kasoro za kutosha," anahitimisha.
Mnamo mwaka 2019, uchunguzi wa mauaji ya Agnes Wanjiru ulizinduliwa, lakini matokeo yake hayakuwekwa wazi. Mnamo mwaka 2021, Gazeti la kila wiki la Uingereza The Sunday Times lilichapisha ushuhuda kutoka kwa askari wanaodai kusikia ungamo la mwenzao. Ushahidi ulikataliwa.
"Tunaendelea kujitolea kusaidia [familia ya Agnes Wanjiru] kupata haki," msemaji wa serikali ya Uingereza alisema katika taarifa.
Ombi la kurejeshwa bado linaweza kuchukua miaka kadhaa kushughulikiwa. Familia ya Agnes Wanjiru na mawakili wake watakuwa Uingereza mwanzoni mwa mwezi Oktoba kufikiria kuwasilisha malalamishi nchini humo.