WATAALAMU wa ugani nchini wametakiwa kufikisha kwa wananchi elimu ya usimamizi wa misitu, ili suala la usimamizi endelevu wa misitu, kitalu cha miti, ufugaji nyuki, uongezaji thamani na teknojia ya kuongeza thamani mazao ya misitu na nyuki iwe endelevu na kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu.
Kamishna wa Uhifadhi TFS, Dos Santos Silayo, amesema hayo kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Revocatus Mushumbusi, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi misitu kwa maofisa ugani kutoka TFS yaliyoandaliwa na Timu ya wanasheria watetezi wa mazingira kwa vitendo (LEAT) kwa Shirika la Kuhifadhi Mpingo na maendeleo (MCDI) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (WWF).
Anasema teknolojia hizo zitasaidia wananchi kuongeza kipato na kupunguza kasi ya ukataji miti inayochangia suala zima la uharibifu wa mazingira nchini.
Ofisa Msaidizi wa ufuatiliaji na tathmini wa mradi wa mbinu jumuishi za maboresho ya mnyororo wa thamani ya nishati miti nchini kutoka Timu ya wanasheria waetetezi wa mazingira kwa vitendo (LEAT), Mary Kessy, anasema mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa katika Mikoa 6 ambayo ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro, Tabora na Mwanza.