Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza siku ya Alhamisi kuwa wagonjwa 48 wa Ebola wamethibitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na watu 31 wamefariki baada ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
"Imepita wiki mbili tangu serikali ya DRC itangaze mlipuko wa Ebola... Hadi sasa, kesi wagonjwa 48 waliothibitishwa na wanaowezekana kuambukizwa wameripotiwa, na watu 31 wamefariki," Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amewaambia waandishi wa habari kkwa njia ya video kutoka makao makuu ya WHO huko Geneva.
Mlipuko huo, wa kwanza nchini DRC katika kipindi cha miaka mitatu, ulitangazwa mapema mwezi Septemba.
Misitu minene ya mvua ya Kongo ni hifadhi ya asili ya virusi vya Ebola, ambayo husababisha homa, maumivu ya mwili, na kuhara, na inaweza kuendelea katika miili ya walionusurika na kutokea tena miaka kadhaa baadaye.
Siku ya Jumapili Shirika la Afya Duniani lilitangaza kwamba limeanza kutoa chanjo kwa wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele na mawasiliano ya watu walioambukizwa virusi vya Ebola katika mkoa wa Kasai nchini Kongo, ambapo mlipuko umetangazwa. WHO imesema dozi 400 za awali za chanjo ya Ervebo dhidi ya Ebola, kutoka katika dozi 2,000 zilizohifadhiwa nchini humo, zimewasilishwa huko Bulape, kitovu cha mlipuko huo.
WHO imekabidhi zaidi ya tani 14 za vifaa muhimu vya matibabu, kusambaza wataalam, na kuanzisha kituo cha matibabu ya Ebola ambapo wagonjwa 16 wanatibiwa kwa sasa, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema.
Zaidi ya watu 900 waliotangamana na wagonjwa wa Ebola wametambuliwa na wanafuatiliwa.
Wagonjwa wawili wa kwanza waliopona waliruhusiwa kutoka hospitalini siku ya Jumanne, ameongeza. Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vimetoa ushauri wa afya siku ya Alhamisi, na kushauri mashirika ya afya ya umma, maabara ya kliniki, na wahudumu wa afya kuhusu mlipuko wa Ebola nchini Kongo.
Kwa sasa, hakuna wagonjwa wanooshukiwa, wanaowezekana au waliothibitishwa kuhusishwa na mlipuko huo wameripotiwa nchini Marekani au nje ya Kongo, shirika hilo limesema, na kuongeza kuwa "hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo nchini Marekani inachukuliwa kuwa ndogo kwa wakati huu."