Marekani yapiga kura ya turufu azimio la UNSC kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano Gaza

Marekani kwa mara nyingine tena imepinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi lililotaka kusitishwa mara moja na katika hali ya kudumu kwa mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka, ikisema kwamba juhudi hizo hazikufika mbali vya kutosha kulaani Hamas.

Wajumbe wengine 14 wa chombo chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa walipiga kura kuunga mkono azimio hilo, ambalo linaelezea hali ya kibinadamu huko Gaza kuwa "janga" na kuitaka Israel kuondoa vikwazo vyote vya kupeleka misaada kwa Wapalestina milioni 2.1 wa eneo hilo.

"Upinzani wa Marekani kwa azimio hili hautashangaza," amesema Morgan Ortagus, mshauri mkuu wa sera za Marekani, kabla ya kupiga kura. "Umoja wa Mataifa haulaani Hamas wala hautambui haki ya Israel ya kujilinda, na unahalalisha kimakosa masimulizi ya uongo ambayo yananufaisha Hamas na ambayo kwa bahati mbaya yamepata mashiko ndani ya Baraza hili." Ameongeza kuwa wajumbe wengine wa Baraza "wamepuuza" maonyo ya Marekani kuhusu lugha hii "isiyokubalika" na badala yake wakachukua "hatua ya kiutendaji inayolenga kupata kura ya turufu."

Matokeo haya yanasisitiza zaidi kutengwa kwa kimataifa kwa Marekani na Israel juu ya vita vya Gaza vinavyodumu kwa takriban miaka miwili. Kura hiyo imekuja siku chache kabla ya mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa dunia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo Gaza itakuwa suala kubwa na washirika wakuu wa Marekani wanatarajiwa kutambua taifa huru la Palestina. Ni hatua ya kiishara ambayo Israel na Marekani zinapinga vikali, na kuugawanya utawala wa Trump na washirika wake, zikiwemo Uingereza na Ufaransa.

Azimio la hivi punde liliweka usitishaji vita kuwa na masharti ya kuachiliwa kwa mateka.

Likiwa limeandaliwa na wajumbe kumi wa Baraza, waliochaguliwa kwa muhula wa miaka miwili, azimio hili linakwenda mbali zaidi kuliko matoleo ya awali na kuangazia kile linachokiita "mateso yanayozidi" ya raia wa Palestina.

"Ninaelewa hasira, kufadhaika, na kukatishwa tamaa kwa watu wa Palestina ambao wanafuatilia kikao hiki cha Baraza la Usalama, wakitumai kwamba msaada uko njiani na kwamba jinamizi hili linaweza kuisha," mesemaRiyad Mansour, balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa. 

Algeria, moja ya nchi zilizofanya azimio hilo liwekwe mezani, pia imeeleza kusikitishwa na kushindwa kwa hatua mpya za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza, na kuwaomba radhi Wapalestina kwa kutofanya vya kutosha kuokoa maisha ya raia.

Licha ya kushindwa kwa mpango huu, Balozi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa, Amar Bendjama, amesema: "Wanachama 14 wenye ujasiri wa Baraza la Usalama walitoa sauti zao. Walitenda kwa uangalifu na katika huduma ya maoni ya umma ya kimataifa."

Balozi wa Pakistan ameita kura hiyo, ambayo ilifanyika wakati wa mkutano wa 10,000 wa Baraza la Usalama, "wakati wa giza."

Danny Danon, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, amekosoa vikali mpango huu mpya, akisema "hautawaachia huru mateka au kuleta usalama katika eneo hilo."

"Israel itaendelea kupambana na Hamas na kuwalinda raia wake, hata kama Baraza la Usalama litapendelea kufumbia macho ugaidi," amesema katika taarifa yake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii