Wananchi wa Guinea wanapiga kura ya ndiyo au hapana kuhusu rasimu ya Katiba mpya. Rasimu hiyo inalenga kuchukua nafasi ya katiba ya mpito inayotumika tangu mapinduzi ya Septemba 21, 2021 ambayo yalishuhudia Mamadi Doumbouya akimpindua rais Alpha Condé. Zaidi ya wapiga kura milioni 6.5 kati ya milioni 14.5 nchini humo wanatarajiwa kupiga kura zao. Uchaguzi huu unaashiria hatua muhimu katika mpito kuelekea kurejea kwa utaratibu wa kikatiba.
Nchini Guinea, suala kuu ni kurejea kwa utaratibu wa kikatiba na mwisho wa mpito wa kuruhusu nchi hiyo kuungana tena na mashirika ya kikanda na kimataifa, anaripoti mwandishi wetu wa Conakry, Moktar Bah. Rasimu ya Katiba mpya ina ibara 199. Rasimu hii inaonwa na watetezi wake kama chombo cha kupatanisha taifa na siku zake zilizopita na kuweka misingi ya uchaguzi wa urais, wa wabunge na serikali za mitaa ifikapo mwisho wa 2025 au mapema 2026. Rasimu hiyo inaleta ubunifu kama vile huduma ya afya kwa wote, hakikisho la haki ya elimu bure hadi shule ya upili, na mbinu za kudhibiti ufisadi. Rasimu hiyo pia inatoa haki zilizoimarishwa katika elimu na afya, pamoja na kuongezeka kwa ugatuaji ili kupunguza mivutano ya kikabila na kikanda na kuunganisha umoja wa kitaifa baada ya miaka kadhaa ya mgogoro.
Ikikubaliwa, Rasimu hii ya katiba mpya itahifadhi yaliyotekelezwa kwa ujumla na watangulizi wake. Kwa hivyo, utawala wa Guinea utabaki kuwa wa kirais, huku muundo wa serikali na mgawanyo wa madaraka ukisalia sawa, isipokuwa taasisi mbili mpya: Bunge la Seneti, na wajumbe waliochaguliwa kwa miaka sita, lakini theluthi moja kati yao watateuliwa moja kwa moja na mkuu wa nchi. Na Mahakama Maalumu ya Haki ya Jamhuri, “yenye uwezo wa kumshtaki rais na wajumbe wa serikali katika kesi za uhaini mkubwa, uhalifu na makosa” waliyotenda katika kipindi chao.
Muda wa uongozi wa Mkuu wa Nchi utaongezwa hadi miaka saba, ambayo inaweza kuongezwa mara moja. Kuanzia sasa, wagombea binafsi watakuwa na haki ya kugombea katika uchaguzi wa urais. Kuhusu usawa wa kijinsia, 30% ya nyadhifa za kuchaguliwa na za umma lazima zihifadhiwe kwa wanawake. Jambo lingine: Ibara ya 74 ya rasimu ya katiba inawapa marais wa zamani "kinga ya kiraia na ya jinai kwa vitendo walivyofanya katika kutekeleza majukumu yao mara kwa mara."
Viongozi wa upinzani na makundi mengine wanatoa wito wa kususia kura hii ya maoni. Wanashutumu Rasimu ya Katiba kwamba ililitengenezwa kwa ajili ya Mamadi Doumbouya, ambayo itamuwezesha kugombea katika uchaguzi ujao wa urais. Washiriki wa uchaguzi wa Jumapili hii kwa hivyo wataangaliwa kwa karibu, anaripoti mwandishi wetu maalum huko Conakry, Léa-Lisa Westerhoff. Hiki kitakuwa kiashiria kikuu cha iwapo Waguinea wanavutiwa na wito wa mamlaka wa kupitisha Katiba hii mpya, baada ya kampeni isiyo na mvuto ambapo wafuasi wa rasimu hii ya Katiba pekee ndio walisikika.
Suala jingine, hatimaye, linahusishwa moja kwa moja na muktadha wa usalama. Mnamo mwaka 2020, kura ya maoni juu ya katiba mpya - ambayo ilipaswa kuruhusu Alpha Condé kugombea muhula wa tatu - ilisababisha vifo vya watu kadhaa katika hali ya mvutano mkubwa. Siku ya Ijumaa, mkuu wa kikosi cha askari katika ngazi ya taifa, Balla Samoura, alitangaza kutumwa kwa askari 45,000 wa vikosi vya ulinzi na usalama na ndege zisizo na rubani ili kulinda mchakato wa uchaguzi. Karibu waangalizi 6,000 kutoka mashirika ya kiraia ya Guinea pia watatumwa kwenye vituo takriban 23,600 vya kupigia kura nchini humo. Wanaahidi kuripoti hitilafu zozote zitakazojitokeza katika mchakato wa uchaguzi.