ICC yamkuta na hatia aliyekuwa mbabe wa kivita nchini Sudan Ali Kushayb

Mahakama ya kimataifa ya ICC, imemkuta na hatia ya makosa ya uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya binadamu, aliyekuwa muasi na mbabe wa kivita nchini Sudan, Ali Muhammad Ali Abdi-Rahman, uhalifu alioutekeleza kwenye jimbo la Darfur.

Al-Rahman anayefahamika kwa jina jingine kama Ali Kushayb, alikutwa na hatia ya makosa yote aliyoshtakiwa nayo, ikiwemo ubakaji, mauaji na mateso, vitendo alivyotekeleza kati ya Agosti 2003 na April 2004.

Akisoma uamuzi wao, jaji kiongozi Joanna Korner, amesema upande wa mashtaka umethbitisha pasipo na shaka makosa ambayo mtuhumiwa alikuwa ameshtakiwa nayo, ambapo hukumu ya adhabu atakayopewa itatolewa siku nyingine.

Awali Al-Rahman alikuwa amekana kujulikana kwa jina la Ali Kushayb, utetezi ambao majaji waliutupilia mbali baada ya kujiridhisha kuwa alikuwa pia akitumia jina hilo. 

Kushayb alikimbilia Jamuhuri ya Afrika ya Kati mwezi Februari mwaka 2020 wakati serikali mpya ya Sudan ilipotangazwa na kuahidi kushirikiana  na mahakama ya ICC.

Machafuko yalizuka Darfur baada ya raia wasio waarabu kulalamika kuuawa na kutengwa ambapo walianzisha uasi uliojibiwa na utawala wa Khartoum uliotumia kundi la Janjaweed kukabiliana nao.

Umoja wa Mataifa unasema watu laki 3 waliuawa na wengine Zaidi ya milioni 2 walikosa makasi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii