Umoja wa Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na taasisi zinazoongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na C-Sema na Elimika, wameandaa mwongozo wa uandishi wa habari za ukeketaji ikiwa lengo la mwongozo huo ni kusaidia kukomesha ukatili wa kijinsia ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia kuhusu mwongozo huu, Victor Maleko kutoka UTPC amesema kuwa mwongozo huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wanahabari kwa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari ya kitaalamu na haki za walengwa.
Aidha, alisema kuwa utasaidia katika kuandika habari za ukeketaji kwa usahihi na kwa kuzingatia muktadha wa kijamii.
Kwa upande mwingine, James Massawe, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Elimika, pamoja na Fatuma Kamramba, Mkurugenzi wa Miradi kutoka C-Sema, wamesema kuwa tafiti walizofanya zimedhihirisha umuhimu wa kuwajengea uwezo wanahabari ili waandishi waweze kuandika habari za ukeketaji kwa weledi. Massawe alisema, "Mwongozo huu utapatikana kwenye kitabu na utatolewa kwa kila Press Club kwa matumizi ya wanahabari. Tunatarajia kutoa pia elimu zaidi kuhusu masuala ya uandishi wa habari na makala za ukeketaji ili kufikia malengo yetu."
Hata hivyo Azizi Msuya ambaye ni mwandishi wa habari kutoka Morogoro, amewashauri wanahabari nchini kulichukulia suala la ukatili wa kijinsia kama ajenda ya kitaifa. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wanahabari kuhakikisha wanalisimamia kwa weledi ili kutunga sera zinazolenga kuongeza juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia, na hatimaye kufikia malengo ya kutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2030.
Aidha mwongozo huo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii, serikali, na wadau mbalimbali kushirikiana katika kutokomeza ukeketaji na ukatili mwingine wa kijinsia, na kuleta mabadiliko katika jamii.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime