Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu ameshiriki uzinduzi wa shughuli za ujenzi wa mgodi wa madini ya kinywe (graphite) uliofanywa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde katika hafla iliyofanyika Oktoba 9 mwaka katika eneo la Mahenge Wilaya ya Ulanga Mkoa wa Morogoro.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Faru Graphite Corporation kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (hisa 16%) na Black Rock Mining Limited (hisa 84%) ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya madini nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhe. Mavunde alisema ujenzi wa mgodi huo unatarajiwa kugharimu takribani $510 milioni (zaidi ya Sh1.3 trilioni).
Aliendelea kusema kuwa uwekezaji huo utazalisha ajira zaidi ya 400 wakati wa ujenzi na zaidi ya 900 za kudumu mgodi utakapoanza uzalishaji kamili.
Nje ya mgodi alisema Mhe. Mavunde ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 4,500 zinatarajiwa kuchochewa kupitia mnyororo wa thamani wa wachuuzi wakulima wasambazaji wa bidhaa na watoa huduma.
Ingawa serikali inatarajia kupata zaidi ya $3.2 bilioni (zaidi ya Sh7 trilioni) katika kipindi cha uhai wa mgodi---miaka 26 kupitia kodi, tozo, gawio, na mrabaha wa madini.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Faru Graphite Corporation alisema kuwa Serikali kupitia ubia huu inalinda maslahi ya taifa huku ikinufaika kupitia hisa, kodi, ajira na mzunguko wa fedha.
Ingawa aliongeza kuwa mradi huo utachangia kuimarisha uchumi wa taifa kwani sehemu kubwa ya madini itauzwa nje ya nchi hivyo kuongeza mapato ya kigeni kuendeleza biashara za ndani na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi wa eneo husika na mikoa jirani.
Pia alibainisha kuwa uwekezaji kama huo unasaidia kuimarisha sekta ya madini na kufanya Tanzania kuwa kitovu cha malighafi za teknolojia safi barani Afrika.
“Tumejizatiti kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kukuza uchumi wa taifa inatimia, hususan kupitia sekta ya madini na uwekezaji wa kimkakati,” alisema Bw. Mchechu.