Mfanyabiashara maarufu na bilionea Chief Jite Odeworitse Tesigimoje, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GIM Brown Marine, ameibua mjadala mkubwa nchini Nigeria baada ya kufunga ndoa na mke wake wa 19 katika sherehe iliyofanyika kwa kifahari katika kijiji chake cha Ugborodo, jimbo la Delta.
Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 43, anayejulikana kwa kauli zake zenye utetezi wa ndoa za wake wengi, amesema kwamba mfumo huo ni sehemu ya utamaduni wa Kiafrika na ukweli wa kibinadamu, si dalili ya anasa.
“Kila mwanaume angependa kuoa wake wawili au watatu kama ana uwezo,” alisema Tesigimoje. “Wakati mahusiano yanapozoeleka, hisia hupungua. Ndoa za wake wengi hurejesha msisimko na uwiano.”
Amesema familia yake, inayojumuisha wake kutoka makabila makubwa ya Nigeria, ni mfano wa umoja na ujumuishi.
Akikosoa mfumo wa ndoa za mke mmoja, Tesigimoje alisema ni wazo lililoletwa na ukoloni, na si sehemu ya asili ya jamii za Kiafrika.
“Wakoloni walitufundisha kuwa ndoa ya mke mmoja ndiyo bora, lakini jamii zao pia zimejaa changamoto za maadili. Kama mwanaume anamvutiwa na mwanamke mwingine, ni bora kumuoa kuliko kuishi kwa unafiki,” alisema.
Bilionea huyo alisema anahakikisha usawa na haki kwa wake zake wote, akiwapatia kila mmoja nyumba ya vyumba vitano, posho na haki sawa.
“Uadilifu ndio siri ya amani nyumbani. Nikipa mmoja ₦250,000, wote wanapata kiasi hicho hicho,” aliongeza.
Sherehe yake ya hivi karibuni ilihudhuriwa na wake zake wote 19, waliovaa mavazi yanayofanana kama ishara ya umoja wa kifamilia.
Hata hivyo, Tesigimoje alikiri kuwa mfumo wa ndoa za wake wengi si kwa kila mtu, akisisitiza kuwa unahitaji uwezo wa kifedha na ustahimilivu wa kihisia.
“Ndoa za wake wengi zinahitaji busara na uwajibikaji mkubwa. Huwezi kumtelekeza yeyote,” alisema.