WIZARA ya Maliasili na Utalii imeweka mikakati madhubuti katika utekelezaji wa Sera mpya ya Misitu na Ufugaji Nyuki ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wizara za kisekta, taasisi binafsi na jamii kwa ujumla kwa manufaa ya maendeleo endelevu ya taifa.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 10 mwaka huu jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa wizara hiyo Seleboni Mushi wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau na wizara za kisekta kilichojadili changamoto na fursa katika maendeleo ya sekta ya misitu nchini.
Amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia sekta hiyo ikiwemo mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ukuaji wa pato la taifa, na kuongeza ajira bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji ushirikiano wa pamoja katika kuzitatua.
“Sekta hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na shughuli za kibinadamu, zikiwemo uvunaji haramu wa mazao ya misitu, uingizaji wa mifugo katika hifadhi, uanzishwaji wa mashamba ya kilimo, na uchimbaji wa madini usiozingatia taratibu,” amesema Mushi.
Aidha amesema Wizara imeendelea kutekeleza programu mbalimbali za upandaji miti na urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika kwa kushirikiana na wadau wote wakiwemo Serikali Kuu ,Serikali za Mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla.