Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekabidhi Vyuo vinne vya Ufundi Stadi na Huduma kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) vilivyopo Njombe, Simiyu, Rukwa na Geita, kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 19.13
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Oktoba 9 mwaka huu mkoani Njombe, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Frederick Salukele, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kuchangia katika uchumi wa nchi.
Vile vile Selukele ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za mafunzo kupitia VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii (FDC) ili kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa VETA, CPA Anthony Kasore, ameshukuru Serikali kwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu na vifaa vya kisasa, huku akisema vyuo hivyo vitatoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya karne ya 21.