Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Songea Damian Dallu aatangaza kuhusu tukio la kutoweka kwa Padri Camillus Nikata wa Jimbo Kuu la Songea ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) Mwanza.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo Askofu Dalu amesema kuwa Padri Camillus haonekani wala hapatikani kwenye simu yake.
"Padri Nikata alikuwa ametokea Dodoma kwenye mafundisho ya moyo ya mapadri wanaofundisha katika Vyuo vikuu vya TEC, akiwa na mhadhiri mwenzake, ambaye ni Padri wa Jimbo hili.
Ambapo alieleza kuwa Padri huyo akiwa Songea alikaa katika nyumba ya mapadri ya St. Vianney na alikuwa amepanga kusafiri kwenda Mwanza Oktoba 8 mwaka huu kwa basi la SUPERFEO ambapo tiketi alishainunua kwa njia ya mtandao.
Aidha Askofu Dallu ameongeza kuwa walianza kuhisi Jumatano mchana kwamba hakusafiri kwenda Mwanza kwani katika chumba chake kilichokuwa kimefungwa ilionekana mizigo yake ambayo alikuwa ameiandaa kwa ajili ya safari.
"Mtumishi wa nyumba ya mapadri alishangaa kwamba mzigo ambao Padri ilitakiwa auchukue toka kwake haukuchukuliwa. Pia mlango wa chumba ulifungwa, lakini ufunguo haukurudishwa kwa mtumishi."
"Baada ya kuona hayo tulianza kumtafuta kwa simu na kwa kuulizia kwa watu aliokaa nao katika nyumba ya mapadri. Hata hivyo hatukufaulu kupata chochote, maana hakupatikana kwa simu na watu hawakujua alikokwenda. Kule Mwanza alikotakiwa kwenda, nako haonekani na hapatikani. Ofisi ya SUPERFEO ilidhihirisha kuwa Padri Nikata alinunua tiketi lakini hakusafiri kwa basi lile." Ameongeza.
Askofu Dallu amesema kuwa baada ya kushindikana kwa jitihada za kumtafuta kila mahali ambapo walidhani angeweza kuwepo, wamepeleka taarifa Polisi kwa msaada zaidi.