Wataalamu wa usalama mtandaoni kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WMTH) kwa kushirikiana na wizara na taasisi za umma, wameendesha mafunzo maalum kwa masheha wa shehia za Zanzibar Oktoba 23 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwezi wa Uhamasishaji wa Matumizi Salama Mtandaoni kwa 2025.
Katika mafunzo hayo, wataalamu hao wamewaasa masheha kuhakikisha wanazingatia ulinzi wa watoto mtandaoni kwa kufuatilia matumizi ya vifaa vya kielektroniki wanapovikabidhi kwao, kwani vifaa hivyo vimekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa maadili na usalama wa taarifa.
Aidha masheha wamekumbushwa kuwa makini na ujumbe wa kitapeli (phishing messages) unaoweza kutumwa kupitia mitandao ya kijamii au simu za mkononi, wakihimizwa kuthibitisha taarifa kabla ya kutoa ushirikiano wowote na kutuma ujumbe wa aina hiyo kwa namba maalum 15040 kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Wataalamu hao wamewataka washiriki kufuata mbinu mbalimbali za kujilinda dhidi ya uhalifu wa mtandao, ikiwemo kutumia nywila imara na kuzibadilisha mara kwa mara, kutotumia nywila moja kwa akaunti nyingi tofauti, kuepuka kubofya viungo visivyojulikana kwenye barua pepe au mitandao ya kijamii, kuweka two-factor authentication (2FA) kwenye akaunti muhimu, na kusasisha mifumo ya vifaa vya kielektroniki mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi.
Vilevile wamewashauri kutumia antivirus na firewalls kulinda taarifa binafsi na data za ofisi, kutochapisha taarifa nyeti kama namba ya kitambulisho au picha binafsi kwenye mitandao ya kijamii, na kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya wazi ya intaneti (public Wi-Fi) hasa wakati wa kufanya miamala ya kifedha. Wameongeza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa jamii kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu mbinu mpya za kitapeli na njia sahihi za kujilinda.
Masheha waliohudhuria mafunzo hayo wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mpango huo wa elimu, wakisema wamepata maarifa muhimu ambayo watayatumia kuelimisha na kulinda jamii zao dhidi ya vitendo vya uhalifu mtandaoni.