Wanafunzi waliotekwa nyara Niger waachiwa huru

Serikali ya Nigeria imethibitisha kuachiwa huru kwa wanafunzi wote waliotekwa nyara katika shule ya St. Mary’s iliyopo katika jimbo la kaskazini la Niger. Taarifa hiyo imetolewa na msemaji wa Ikulu ya nchi hiyo kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X bila  kufafanua namna zoezi hilo lilivyofanikishwa.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, kuachiwa kwa wanafunzi hao kunahitimisha juhudi za serikali za kuwarejesha nyumbani wanafunzi wote waliokuwa wametekwa nyara kutoka shule hiyohivyo serikali haijatoa maelezo kuhusu iwapo kulihusisha operesheni ya kijeshi au malipo ya fedha za kikomboleo.

Aidha tukio la utekaji nyara lilitokea mapema mwezi huu ambapo zaidi ya wanafunzi 300 walichukuliwa mateka na watu wenye silaha. Hadi sasa, takriban wanafunzi 100 walikuwa tayari wameachiwa huru katika awamu ya kwanza ya operesheni ya uokoaji.

Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni Nigeria imekuwa ikikumbwa na wimbi la utekaji nyara hasa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, unaofanywa na wanamgambo wa itikadi kali pamoja na magenge ya majambazi kwa lengo la kujipatia fedha za kikomboleo ambapo serikali ya Nigeria imekuwa ikiahidi kuongeza juhudi za kiusalama ili kukabiliana na vitendo hivyo vinavyoathiri usalama wa raia, hususan wanafunzi wa shule.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii