Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara ya Kilimo, Bw. James Kibamba, amewataka Wataalamu wa udongo nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na umakini ili kuhakikisha matokeo ya upimaji wa udongo yanakuwa sahihi na yenye manufaa kwa taifa.
Akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Wataalamu wa udongo Oktoba 23 mwaka huu Jijini Dodoma Bw. Kibamba amesema upimaji wa udongo ni nguzo muhimu katika kupanga matumizi bora ya ardhi na kuongeza tija ya uzalishaji wa kilimo nchini.
Amesema nchi zilizoendelea kama China, India na Misri zimepiga hatua kubwa katika Sekta ya Kilimo kutokana na tafiti sahihi za udongo, ambazo zimewezesha kulima mazao yanayolingana na hali ya ardhi ya maeneo husika.
Kwa mujibu wa Bw. Kibamba upimaji wa udongo kwa mwezi huu unatekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Mara na Kagera, kabla ya kuendelea mwezi ujao katika Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, na kumalizika Desemba katika Tanga, Pwani, Lindi, Morogoro na Mtwara.
Ameeleza kuwa kazi hiyo inalenga kupata ramani za kidijitali zenye kipimo cha 1:50,000 zitakazosaidia kutoa mwongozo sahihi wa matumizi ya ardhi na mbolea kwa kila ekolojia ya kilimo, hatua itakayoiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee barani Afrika.
Hadi sasa upimaji huo umekamilika katika mikoa 10 ikiwemo Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, Geita na Simiyu, na Serikali imeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada hizo ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakua kwa msingi wa taarifa sahihi za udongo.