Kuelekea kongamano la Kimataifa kuhusu amani kwenye ukanda wa Maziwa Makuu litakolofanyika siku ya Alhamisi jijini Paris, mashirika kumi na mawili yasiyokuwa ya kiserikali na yale ya kutoa misaada ya kibinadamu, yametoa ombi la pamoja kwa jumuiya ya Kimataifa kuhusu nchi ya DRC.
Mashirika hayo yakiongozwa na Oxfam na World Vision, wanataka hatua za haraka kuchukuliwa ili kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu inayoendolea kushuhudiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Aidha, Mashirika hayo yamesema kuwa, dunia inapaswa kuangalia kwa undani hali mbaya inayoshuhudiwa katika maeneo yanayokabiliwa na utovu wa usalama, ambapo watu hawana chakula na dawa.
Wadau watakaohudhuria kongamano hilo jijini Paris, wamehimizwa kutanguliza hali mbaya ya kibinadamu mashariki mwa DRC na kuja na majibu ya kuwasaidia maelfu ya watu ambao wanahangaika.
Hapo awali, mashirika ya kibinadamu yalikuwa yameomba Dola Bilioni 2.5 kusaidia, kuwasaidia watu waliothiriwa na vita, ni Dola Milioni 500 ndizo zilizopatikana mpaka sasa.