Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV ametoa wito siku ya Jumapili, Novemba 23, wa kuachiliwa "mara moja" kwa wanafunzi na walimu zaidi ya 300 waliotekwa nyara na watu wenye silaha kutoka shule ya Kikatoliki nchini Nigeria, katika moja ya matukio makubwa zaidi ya utekaji nyara nchini humo. Wanafunzi hamsini kati ya waliotekwa nyara walifanikiwa kutoroka, chama cha Wakristo nchini Nigeria kimetangaza katika taarifa siku ya Jumapili.
"Nimepata taarifa za kuhuzunisha kuhusu utekaji nyara wa makasisi, waumini, na wanafunzi nchini Nigeria," amesema.
Siku ya Jumamosi chama cha Wakristo nchini Nigeria (CAN) kiliripoti kwamba wanaume wenye silaha waliwateka nyara watu 315, wanafunzi na walimu, kutoka shule ya Kikatoliki magharibi mwa Nigeria siku ya Ijumaa, baada ya tukio kama hilo mapema wiki katika shule ya upili kaskazini magharibi mwa nchi (wasichana 25 walitekwa nyara).
Huu ni moja ya matukio muhimu zaidi ya utekaji nyara katika miaka ya hivi karibuni, katika eneo ambalo mara kwa mara hulengwa na makundi ya wahalifu yanayoendesha harakati zao msituni. Asubuhi ya Jumapili hii, Papa Leo XIV, akizungumza kutoka Vatican, alitoa wito wa kuachiliwa huru mara moja kwa wanafunzi hao.
"Ninatoa wito wa dharura wa kuachiliwa huru mara moja kwa mateka," ameongeza Leo XIV, akielezea "huzuni yake kubwa, haswa kwa vijana wengi wa kiume na wa kike waliotekwa nyara na kwa familia zao ziko katika hali nzito." "Tuwaombee ndugu na dada zetu na kwamba makanisa na shule ziweze kubaki mahali salama na penye matumaini," alihitimisha mwishoni mwa sala ya Angelus.
Nimehuzunika sana kusikia kuhusu utekaji nyara wa makuhani, waumini, na wanafunzi nchini Nigeria na Cameroon. Ninahisi huzuni kubwa, haswa kwa vijana wengi wa kiume na wa kike waliotekwa nyara na kwa familia zao zilizo na uchungu. Ninatoa wito wa dhati wa kuachiliwa huru mara moja kwa mateka na kuzitia moyo mamlaka husika kuchukua hatua zinazofaa na kwa wakati unaofaa ili kuhakikisha kuachiliwa kwao. Tuwaombee ndugu na dada hawa na kwamba makanisa na shule ziweze kubaki mahali salama na penye matumaini kila wakati.
Wanafunzi hamsini miongoni mwa zaidi ya 300 waliotekwa nyara siku ya Ijumaa walitoroka watekaji wao, chama cha Wakristo nchini Nigeria kilitangaza katika taarifa Jumapili. "Tumepokea habari njema: wanafunzi 50 wametoroka na kuunganishwa tena na wazazi wao," Chama cha Wakristo nchini Nigeria kilisema katika taarifa, kikibainisha kwamba walitoroka kati ya Ijumaa na Jumamosi.
Wavulana na wasichana waliotekwa nyara kutoka shule ya St. Mary, wenye umri wa miaka 8 hadi 18, wanawakilisha karibu nusu ya wanafunzi 629 wa shule hiyo.
Utekaji nyara huu unakuja baada ya kundi lingine la watu wenye silaha kuvamia shule ya upili katika jimbo jirani la Kebbi siku ya Jumatatu, na kuwateka nyara wasichana 25. Siku iliyotangulia, waumini Wakristo wapatao 30 walitekwa nyara huko Eruku, Jimbo la Kwara. Matukio haya yanachochea hofu ya usalama katika nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika na yamesababisha kufungwa kwa tahadhari kwa shule nyingi kote nchini.
Utekaji nyara huu wa watu wengi ulitokea huku Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni akitishia kuingilia kijeshi nchini Nigeria kutokana na kile alichokiita mauaji ya Wakristo yanayotekelezwa na Waislam wenye msimamo mkali. Mamlaka ya Nigeria imesisitiza kwamba mauaji ya wanajihadi na magenge ya wahalifu yanawaathiri Wakristo na Waislamu kiholela, ambao kila upande mmoja unawakilisha takriban nusu ya raia.
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu amesema "anafurahi" kuona wanafunzi 51 kutoka shule ya Kikatoliki katika Jimbo la Niger wamepatikana. Pia ametangaza kuachiliwa kwa makasisi 38 Wakristo waliotekwa nyara huko Eruku, Jimbo la Kwara, siku ya Jumanne, Novemba 18.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime