Wananchi watakiwa kudumisha umoja na kuepuka mifarakano ya kidini,kikabila na kisiasa

Wananchi wametakiwa kutojikuta wakigawanyika kwa misingi ya kidini, kikabila au kisiasa, badala yake waenzi na kudumisha utambulisho wao kama Watanzania kwa kuwa hilo ndilo linalowaunganisha na kuwapa dira ya pamoja.

Wito huo umetolewa Novemba 23 mwaka huu katika Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, wakati Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Sungusungu, wenyeviti wa serikali za vijiji na viongozi wa tiba asili kutoka tarafa za Ngudu, Nyamilama na Mwamashimba.

Katika hotuba yake, Kamanda Mutafungwa aliwahimiza viongozi hao na wananchi kwa ujumla kutoshiriki au kuruhusu vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani, kwani maendeleo ya Taifa yanategemea mazingira tulivu.

"Unakataje tawi la mti wakati uko juu ya hilo tawi? Ukiliangusha, kweli utapona?" Alihoji Kamanda Mutafungwa, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani iliyopo.

Aidha, aliwataka viongozi hao kwenda kuwakumbusha na kuwaelimisha vijana pamoja na watu wote wanaoshawishika na makundi yenye malengo ya kuvuruga amani. Alisema: "Gharama ya kuitunza amani ni ndogo, lakini gharama ya kuirudisha amani iliyopotea ni kubwa mno. Msichezee amani tuliyonayo."

Alihitimisha kwa kuwasihi vijana kuipenda nchi yao, kuacha mitazamo hasi na kuchukua jukumu la kuitetea Tanzania kwa kila hali.

Kwa upande wao, viongozi walioshiriki mkutano huo mbali na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi waliahidi kuyatekeleza maagizo ya Kamanda.

Mtemi wa Sungusungu Wilaya ya Kwimba, Kanda ya Ziwa na Magharibi, Shimbi Mogani, alisema wamekuwa na utaratibu wa kukutana kila mwisho wa mwezi kujadili namna ya kuimarisha usalama kwa wananchi, hivyo wamefurahia kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kikao hicho.

Naye Agnes Ndenge, mkazi wa Kata ya Mwamashimba, alisema: “Tunaomba nchi yetu iendelee kuwa ya amani. Tumejifunza mengi, tutaenda kuhamasisha amani katika maeneo yetu kama alivyoagiza Kamanda.”

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii