Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya na Mbunge wa Busanda, Dk. Jafari Seif, amewataka watumishi wa afya kote nchini kutumia lugha ya heshima, upole na tabasamu wanapotoa huduma kwa wagonjwa wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Dk. Jafari ameyasema leo mara baada ya kutembelea Kituo cha afya cha Nyarugusu, kilichopo Kata ya Nyarugusu, Jimbo la Busanda, Wilaya ya Geita na kuzungumza na watumishi wa kituo hicho.
“Serikali ya Dk. Samia itaendelea kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo na zahanati. Hata hivyo, pamoja na maboresho hayo, nyinyi watoa huduma mna wajibu wa kumpokea mgonjwa kwa tabasamu na kutumia lugha safi, si lugha chafu,” amesema Dk Jafari.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Fred Feliasianj, amesema kuwa wamefurahishwa na ziara ya Naibu Waziri na kusema kituo hicho kinahudumia wananchi wengi na kinahitaji maboresho zaidi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime