Marekani imesaini mkataba wa msaada wa afya wa dola bilioni 2.5 na Kenya, ambao ni mkataba wa kwanza wa aina hiyo wa pande mbili baada ya Rais Donald Trump kulivunja shirika la misaada la Marekani - USAID.
Maafisa wa utawala wa Trump wamesema makubaliano hayo yatakuwa ya kwanza katika mfululizo wa makubaliano na serikali za nchi zinazoendelea, ambazo zitaombwa kuchangia gharama na kushirikiana na Washington katika vipaumbele vingine.
Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alisaini makubaliano hayo mjini Washington na Rais wa Kenya William Ruto, ambaye alimsifu kwa msaada wake wa ulinzi katika nchi ya Haiti inayokumbwa na matatizo.
Rais Trump alilivunja shirika la kihistoria la USAID na kuyatenga mashirika yasiyo ya kiserikali, hatua iliyokosolewa vikali kote ulimwenguni.
Chini ya makubaliano hayo, Marekani itaipa Kenya dola bilioni 1.6 katika kipindi cha miaka mitano ili kushughulikia masuala ya afya ikiwa ni pamoja na kupambana na VVU na malaria na kuzuia polio.
Kenya itachangia dola milioni 850 nyingine kwa makubaliano ya kuyachukua majukumu mengine zaidi hatua kwa hatua.
Ruto alisema makubaliano hayo yatachangia vipaumbele vya Kenya ikiwemo kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya hospitali na kuimarisha nguvu kazi kwenye sekta ya afya.