Putin afanya ziara ya kihistoria India

Rais wa Urusi Vladimir Putin anaanza ziara ya siku mbili nchini India katika juhudi za kuimarisha ushirikiano hususan katika sekta ya ulinzi. 

Ziara hiyo imefanyika wakati ambao India inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka nchini  Marekani ikiitaka India iachane na ununuzi wa mafuta kutoka Urusi.

Hivyo ziara hii imekuwa ya kwanza kwa kiongozi huyo nchini humo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine  huku akiambatana na  Waziri wa Ulinzi Andrei Belousov.

Rais huyo wa Urusi, anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu Narendra Modi watakaposhiriki pamoja dhifa maalumu ya faragha baadaye jioni. 

Dhifa hiyo itafuatiwa na mkutano pamoja na mazungumzo na wafanya biashara yatakayofanyika Ijumaa.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov awali alieleza kuwa moja ya ajenda muhimu zitakazozungumziwa na viongozi hao wawili katika kuimarisha ushirikiano wa kiusalama ni pamoja na suala la Urusi kuipatia India mifumo ya ulinzi wa anga ya kisasa inayofahamika kama S-400.

Kando ya ushirikiano wa kiusalama mahusiano ya kibiashara yanatarajiwa kuwemo kwenye ajenda ya mazungumzo mjini Delhi huku wizara ya mambo ya nje ikiuelezea ushirikiano kati ya nchi yake na Urusi kuwa ndiyo uhusiano thabiti zaidi katika nyakakati hizi. 

Ziara ya Vladimir Putin inafanyika baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuziwekea ushuru wa asilimia 50 bidhaa nyingi za India mnamo mwezi Agosti mwaka huu. 

Hatua hiyo ilichukuliwa kama adhabu ya India kwa kununua mafuta ya Urusi.

India yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani imekuwa mnunuaji mkubwa wa mafuta hayo ya Urusi kwa bei nafuu na kuokoa mabilioni ya dola. 

Hilo limeipa Moscow soko kubwa inalolihitaji baada ya wateja wake wakubwa wa Ulaya kusitisha kununua mafuta ya Urusi kwa sababu ya vita yake na Ukraine.

Duru za habari zinasema India inahofia kuwa makubaliano mapya ya nishati na usalama na Urusi yanaweza kumkasirisha Trump na matokeo yake yanaweza kuwa mabaya katika mazungumzo ya kibiashara yanayoendelea na Washington. 

Hata hivyo msemaji wa Kremlin amebainisha kuwa Urusi kwa upande wake haijali lolote kuhusu ushuru wa Marekani.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii