Desemba 5 mwaka huu mkoani Geita Katika muendelezo wa ziara yake ya kukutana na watumishi wa sekta ya afya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Ndugu Yefred Myenzi, amefanya kikao maalum na watumishi wa sekta ya afya katika Kituo cha Afya Nyankumbu kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao pamoja na kuhimiza uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Myenzi aliwakumbusha watumishi kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi.
Hivyo aliwataka watumishi wa umma kutambua nafasi zao na kuwa na huruma kwa watu wanaowahudumia kwani wengi wao hukumbwa na changamoto mbalimbali.
Aidha, amekemea tabia ya utoro na ukwepaji majukumu mahali pa kazi, akisisitiza kuwa matokeo ya kazi ndiyo kipimo cha uwajibikaji.
Ameendelea kusisitiza matumizi ya kauli nzuri kwa wagonjwa, kuonyesha heshima, na kuwapa faraja wale wanaofika kutibiwa.
Pia, amewataka watumishi kuwa waaminifu kwa kuepuka kuomba au kupokea rushwa na kuwa viongozi wa mfano kwa jamii.
Kuhusu maendeleo ya kituo hicho, Mkurugenzi amesema Serikali ina mpango wa kujenga uzio katika Kituo cha Afya Nyankumbu ili kuongeza usalama.
Ameonya kuhusu migogoro kazini akisema huathiri utoaji wa huduma na inaweza kusababisha madhara kwa wagonjwa.
Alisisitiza umuhimu wa mshikamano kazini, kupendana, na kushirikiana kama timu. "Mahala pa kazi pasiwe sehemu ya migogoro, bali pawe sehemu ya kujifunza, kusaidiana, na kufurahia kazi," aliongeza.
Kwa upande wao watumishi wa afya walimshukuru Mkurugenzi kwa kusikiliza na kugusa changamoto zao.
Hata hivyo wamemuomba aendelee na ziara za aina hiyo mara kwa mara ili kuimarisha mawasiliano, mshikamano na uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime