Mamlaka ya Benin imetangaza Jumapili kuzima jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililolenga kumuondoa madarakani Rais Patrice Talon Umoja wa Afrika umelaani jaribio hilo huku Jumuiya ya ECOWAS ikituma msaada wa kijeshi.
Hali ilikuwa ya wasiwasi siku ya Jumapili katika mji mkuu wa kibiashara wa Benin - Cotonou, baada ya milio kadhaa ya risasi kusikika na kundi la wanajeshi kutangaza kwenye televisheni ya taifa kumpindua rais Patrice Talon anayemaliza hapo mwakani (2026) muda wake wa miaka 10 madarakani.
Wanajeshi hao walitangaza pia kuifunga mipaka ya nchi hiyo na kumteua Luteni Kanali Pascal Tigri kuwa rais wa kile walichokiita " tume ya mageuzi ya kijeshi."
Hata hivyo jaribio hilo la mapinduzi lilizimwa haraka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Benin Alassane Séidou aliuhakikishia umma kuwa wamefanikiwa kukidhibiti kikundi kidogo cha wanajeshi kilichoanzisha uasi kwa lengo la kuyumbisha serikali na taasisi zake huku akiwataka raia wa Benin kuendelea na shughuli zao.
Baadaye, rais Patrice Talon alilihutubia taifa na kuhakikisha kuwa hali "imedhibitiwa kikamilifu" na kwamba "usalama na utulivu vinashuhudiwa katika eneo lote la nchi hiyo". Aidha Rais Talon aliwapongeza wanajeshi waliofanikiwa kuzima jaribio hilo la mapinduzi:
Umoja wa Afrika umelaani vikali jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi nchini Benin amapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf alikemea vitendo vyote visivyo halali na kuwataka wanajeshi wote kurejea kwa haraka kwenye kambi zao na kuendelea na majukumu yao.
Kwa upande wake Jumuiya ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imetangaza "kupelekwa mara moja" kwa kikosi maalum cha kulinda amani kitakachowajumuisha wanajeshi kutoka Nigeria, Sierra Leone, Ivory Coast na Ghana ili kuiunga mkono "serikali na jeshi" la Benin kwa lengo la "kudumisha utaratibu wa kikatiba".
Taarifa ya ECOWAS ilitolewa baada ya Msemaji wa Jeshi la Anga la Nigeria, Jenerali Ehimen Ejodamen, kutangaza kuwa walituma ndege za kivita nchini Benin ili kusaidia kukabiliana na waasi waliojaribu kuipindua
Katika historia ya siasa za Benin imegubikwa na mapinduzi au majaribio ya mapinduzi kadhaa lakini mapinduzi ya mwisho yalishuhudiwa mwaka 1972 na Patrice Talon aliye madarakani tangu mwaka 2016 atamaliza muhula wake wa pili na wa mwisho mwaka 2026 kulingana na Katiba ya nchi hiyo.
Ingawa anasifiwa kwa kuchangia kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini Benin, rais Talon anashutumiwa na wakosoaji wake kwa kuchukua hatua za kimabavu katika nchi ambayo hapo awali ilisifiwa kwa demokrasia yake imara. Mrithi na mteule wa Talon, ni Waziri wa Fedha wa sasa Romuald Wadagni, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa rais mwezi Aprili 2026, kwani chama kikuu cha upinzani kikiongozwa na rais wa zamani Boni Yayi kimezuiwa kushiriki.
Benin nchi ndogo ya Afrika Magharibi yenye ukuaji imara wa kiuchumi lakini iliyokumbwa na vurugu za makundi ya kigaidi katika eneo lake la kaskazini kama ilivyo kwa mataifa mengi ya eneo hilo.
Pia mataifa mengi ya Afrika Magharibi yanakabiliwa ukosefu wa utulivu wa kisiasa tangu mwanzoni mwa muongo huu huku mapinduzi yakishuhudiwa nchini Mali, Burkina Faso, Niger, Guinea na hivi karibuni huko Guinea-Bissau.
Aidha kulingana na vyanzo vya kijeshi, wanajeshi kumi na wawili wamekamatwa wakiwemo waliohusika na tukio hilo bila hata hivyo kueleza iwapo kiongozi wa waasi hao Luteni Kanali Pascal Tigri, alikuwa miongoni mwa waliokamatwa.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime