Serikali yazuia maandamano, Waziri Simbachawene aonya umma

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene ametoa angalizo kali kwa wananchi kutoshiriki kile kinachoelezwa kama “maandamano ya amani yasiyo na mipaka wala mwisho” yanayohamasishwa mitandaoni na katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri Simbachawene amesema maandamano hayo hayana kibali hawafahamiki waandaaji wake hayafuati utaratibu na hayana mwisho hivyo si halali na yanaonyesha dalili za uvunjifu wa amani na hata viashiria vya mapinduzi.

Amefafanua kuwa serikali imebaini taarifa mbalimbali zinazosambaa mitandaoni kuhusu watu wanaohamasisha maandamano hayo, na kwamba hatua hiyo inahatarisha usalama wa nchi na utulivu wa wananchi.

Waziri Simbachawene pia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuhimiza amani na kuwaongoza waumini, akisema huo ndiyo mwelekeo sahihi unaohitajika katika kipindi hiki.

Aidha amewataka wananchi kuacha hata ile tabia ya kwenda “kuangalia yanayotokea,” kwa kuwa wanaweza kujikuta wanahusishwa na matukio ambayo hawakupanga.

Serikali imesisitiza kuwa haitaruhusu shughuli yoyote inayoashiria uvunjifu wa amani, ikitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha utulivu na kujiepusha na miito isiyo rasmi.

Aidha imeeleza kuwa maandamano hayo hayana uhalali wowote, waandaaji hawajawasilisha barua, hawafahamiki, na hivyo hayakubaliki kisheria.

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene, mtu anayeshabikia maandamano hayo hana uzalendo kwa nchi yake wala haipendi Tanzania.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii