ECOWAS yatuma wanajeshi Benin kufuatia jaribio la mapinduzi

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS)siku ya Jumapili jioni imetangaza kwamba imepeleka wanajeshi nchini Benin kufuatia jaribio la mapinduzi lililozuiwa na mamlaka mapema siku hiyo. Katika taarifa, taasisi hiyo ya kikanda imesema "imeamuru kupelekwa mara moja kwa wanajeshi wa kikosi maalumu," wanajeshi kutoka Nigeria, Sierra Leone, Côte d'Ivoire, na Ghana, ili kuunga mkono "serikali na Jeshi la Jamhuri la Benin" na "kuhifadhi utaratibu wa kikatiba."

Ofisi ya rais wa Nigeria ilithibitisha kwamba jeshi la Nigeria limefanya mashambulizi ya angani huko Cotonou na kupeleka wanajeshi wa ardhini kwa ombi la jirani yake wa Benin, haswa "kulinda utaratibu wa kikatiba" na kukabiliana na jaribio la mapinduzi. Katika taarifa, ofisi ya rais ya Nigeria, imebainisha kwamba Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliagiza ndege za kivita kuingia anga ya Benin ili kusaidia "kuwaondoa wanajeshi waliopanga mapinduzi kutoka kituo cha televisheni ya taifa na kambi ya kijeshi ambapo walikuwa wamekusanyika," pamoja na kupelekwa kwa wanajeshi wa ardhini "nchini Benin."

Kabla ya hotuba ya Talon na taarifa ya ECOWASUfaransa ilikanusha madai yaliyosambazwa kwamba maafisa wa Benin walikimbilia katika ubalozi wake huko Cotonou. "Hakuna ukweli wowote kati madai haya," imeeleza Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, ambayo ilibainisha kwamba ilikuwa ikifuatilia kwa karibu "hali nchini Benin." Paris iliwasihi raia wake nchini Benin kuwa "makini kubwa," ikibainisha kwamba "hali bado ni tete kwa wakati huu."

Umoja wa Afrika (AU) ulisema kwamba unalaani jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Patrice Talon na kutoa wito kwa jeshi kurudi kwenye kambi zao. Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahamoud Ali Youssouf, pia aliwasihi, katika taarifa iliyochapishwa mtandaoni, "wahusika wote waliohusika katika jaribio la mapinduzi kuacha mara moja vitendo vyote haramu" na "kurejea bila kuchelewa kwenye majukumu yao."

Milipuko mikubwa ilisikika katika vitongoji kadhaa

Mapema siku ya Jumapili, wanajeshi kumi na wawili walikamatwa. Waasi hao wengi wao ni kutoka kwa kikosi cha ulinzi wa taifa, angalau wale waliotambuliwa kwenye televisheni, kulingana na mwandishi wetu huko Cotonou, Jean-Luc Aplogan. Walikimbilia katika kambi ya kijeshi huko Togbin, nje kidogo ya Cotonou. Afisa mkuu aliripoti kwamba kambi hiyo ilikuwa imetekwa tena baada ya mashambulizi kadhaa ya anga. Taarifa hii inabaki, katika hatua hii, ikisubiri uthibitisho rasmi.

Wanajeshi walioasi walitoa madai ambayo yalikuwa ya kisiasa, kijamii, na kijeshi. Walishutumu, haswa, kuzorota kwa hali ya usalama kaskazini mwa nchi na kile walichokiona kama kutelekezwa kwa wenzao waliouawa katika vita.

Asubuhi, milio ya risasi ilisikika karibu na bandari na ikulu ya rais. Mkazi mmoja anasimulia mshangao wake: "Msichana wangu mdogo alisema, 'Ee Mama, inasikika kama radi.' Nilimwambia, 'Hapana, sio radi, inasikika kama risasi.' Kwa hivyo tukaenda kulala. Na haikuchukua muda mrefu, dakika tano au kumi."

Wakati wa mchana, mitambo ya kituo cha habari cha serikali cha Benin TV ilizimwa kwa muda kabla ya kuwashwa tena. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Benin, Alassane Seidou, baadaye aliwasihi "watu kuendelea na shughuli zao kama kawaida." Mapema jioni, milipuko mikubwa ilisikika kwa dakika kadhaa katika vitongoji vya Fidjrossè na Togbin.

Maswali mengi bado hayajajibiwa. Jaribio hili la mapinduzi linakuja miezi minne kabla ya uchaguzi wa urais, ambapo Patrice Talon hatawania katika uchaguzi huo. Huko Cotonou, tukio hilo linaonekana kumshangaza kila mtu. Jumapili jioni, wengi wamejiukiza maswali. Kwa nini sasa, miezi michache tu kabla ya uchaguzi wa wazi wa urais?

Kulingana na vyanzo vilivyo karibu na jambo hilo, waasi walikuwa na malalamiko ya kisiasa dhidi ya serikali ya sasa, haswa wakikosoa mtindo wa utawala wanaouona kuwa wa ubaguzi na ambao unawalazimisha watu kukimbilia uhamishoni. Wengi vile vile wanajiuliza ni nani aliweza kupanga jaribio hili la mapinduzi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii