Wimbi jipya la wakimbizi wa Kongo waingia nchini Burundi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Edouard Bizimana amesema zaidi ya Wakongomani 40,000 wamekimbia mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuingia Burundi katika kipindi cha wiki moja tu.

Waziri huyo amebainisha hayo  katika shirika la habari la AFP kuwa zaidi ya Wakongomani 40,000 wamekimbia mapigano nchini mwao na kuelekea Burundi ndani ya wiki moja, huku mamia ya wengine wakivuka mpaka kuelekea Rwanda.

Kwa mujibu wa makadirio ya awali ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, zaidi ya watu 200,000 wamelazimika kuyahama makaazi yao katika mkoa wa Kivu Kusini tangu Desemba tarehe 2.

Mashirika ya misaada yametahadharisha kuwa ongezeko la wakimbizi linaweza kuzidisha mgogoro wa kibinadamu katika ukanda huo, hasa ikizingatiwa kuwa mapigano mashariki mwa Kongo yamekuwa yakiongezeka.

Kuingia kwa mji wa Uvira mikononi mwa waasi wa M23 kunachukuliwa kama pigo jipya kwa serikali ya Kongo.

Vyanzo vya kidiplomasia vya Ulaya vimesema Kongo ina hofu kuwa waasi hao wanaweza kusonga mbele kuelekea mkoa wa Katanga, wenye utajiri mkubwa wa shaba na kobalt, kitovu cha uchimbaji madini ambacho ni tegemeo kubwa la uchumi wa taifa hilo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii