Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatano, Desemba 10, ametangaza kwamba Marekani imekamata meli ya mafuta "kubwa sana" kwenye pwani ya Venezuela, na hivyo kuongeza mvutano na Caracas. Venezuela inaishutumu Washington kwa "wizi wa moja kwa moja."
"Tumekamata meli ya mafuta kwenye pwani ya Venezuela, meli kubwa, kubwa zaidi kuwahi kukamatwa," rais wa Marekani amewaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House. Hakutoa maelezo kuhusu meli hiyo, mmiliki wake, au mahali ilipokuwa ikielekea. "Ilikamatwa kwa sababu nzuri sana," ameongeza, akibainisha kwamba Marekani inakusudia kushikilia meli hiyo.
Mwanasheria Mkuu Pam Bondi baadaye amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba meli iliyokamatwa ilikuwa imebeba mafuta chini ya vikwazo vya Venezuela na Iran. "Kwa miaka kadhaa, meli hii ya mafuta imewekewa vikwazo na Marekani kutokana na kuhusika kwake katika mtandao haramu wa usafirishaji wa mafuta unaounga mkono mashirika ya kigaidi ya kigeni," amesema.
Amebainisha kuwa operesheni hiyo ilifanywa hasa na FBI kwa usaidizi wa Idara ya Ulinzi, akitoa video inayoonyesha wanajeshi wenye silaha wakishuka kutoka kwenye helikopta hadi kwenye sitaha ya meli.
Serikali ya Marekani inaongeza hatua za kiuchumi na kijeshi ili kuongeza shinikizo zaidi kwa kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro. Katika mahojiano ya hivi karibuni na Gazeti la Politico, Donald Trump alisema kwamba siku za Maduro "zinahesabiwa".
Venezuela "inashtumu vikali na kulaani kile ilichokiita wizi usio na aibu na kitendo cha uharamia wa kimataifa, kilichotangazwa hadharani na Rais wa Marekani, ambaye alikiri kushambulia meli ya mafuta katika Bahari ya Karibia," Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela imesema katika taarifa.
Caracas inabaini kwamba kwa "kitendo hiki cha jinai," Rais wa Marekani Donald Trump anaonyesha kwamba "lengo lake limekuwa kukamata mafuta ya Venezuela bila kutoa fidia yoyote, akimaanisha wazi kwamba sera ya uchokozi dhidi ya nchi yetu ni sehemu ya mpango wa makusudi wa kupora rasilimali zetu za nishati."
Kabla ya Washington kutangaza kukamatwa kwa meli ya mafuta ya Venezuela, Rais Maduro alitaka "kukomeshwa kwa uingiliaji kati haramu na wa kikatili wa serikali ya Marekani nchini Venezuela na Amerika Kusini." Kauli hii ya Nicolas Maduro ilitolewa wakati wa maandamano yaliyoandaliwa huko Caracas siku ya Jumatano, Desemba 10, siku ya sherehe ya Tuzo ya Amani ya Nobel huko Oslo kwa kiongozi wa upinzani wa Venezuela MarĂa Corina Machado, ambaye hakuweza kuhudhuria.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime