Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mwanza wamehimizwa kuimarisha ulinzi shirikishi na kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo Yao ya Kibiashara.
Katika kikao kazi kilichofanyika Novemba 24 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mahatma Gandhi, Wilaya ya Nyamagana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amekutana na Viongozi wa Wafanyabiashara Pamoja na wafanyabiashara kutoka wilaya za Nyamagana na Ilemela ikiwa ni katika kujadili hali ya usalama na mikakati ya kuimarisha amani.
Kamanda Mutafungwa alibainisha kuwa madhumuni ya vikao hivyo ni kuongeza ushirikiano kati ya Polisi na wananchi, akisisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja huku akihimiza wafanyabiashara kuhakikisha wanaboresha mifumo ya ulinzi katika maeneo yao, ikiwemo kufunga au kuongeza Kamera za CCTV ili kurahisisha utambuzi na uchukuaji hatua dhidi ya wahalifu.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene, aliwataka wafanyabiashara kutokufumbia macho viashiria vya uhalifu na kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya kamanda wa polisi kwa vitendo, ili kulinda amani na usalama wa mkoa huo.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wamelipongeza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kwa kudhibiti vurugu zilizotokea tarehe 29 hadi 31 Oktoba mwaka huu wakieleza kuwa hatua zilizochukuliwa zilisaidia kurejesha utulivu katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Katika hatua nyingine Wafanyabiashara hao wamesema uwepo wa CCTV Camera umewasaidia kuwatambua baadhi ya wnanchi wenye Nia ovu waliokuwa wakitekeleza Vitendo vya kiharifu Mtaani.
Mkutano huo wa Jeshi la Polisi na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mwanza umefanyika wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likiendelea na kampeni yake ya kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii katika kuimarisha ulinzi.
Na@ Evance Mlyakado
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime