Serikali imesema tukio la Oktoba 29 limeonesha wazi kuwa hakuna idadi ya kutosha ya waandishi wa habari waliobobea katika uandishi wa masuala ya migogoro, vurugu na machafuko, hali ambayo pia iliweka hatarini usalama wa waandishi waliokuwa kazini.
Kutokana na hilo Serikali imejipanga kutoa mafunzo muhimu na endelevu kwa wanahabari ikiwemo mafunzo ya usalama kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
Akitoa salamu za shukrani katika Mkutano wa Waziri Mkuu na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam Prof. Palamagamba Kabudi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema Serikali imejifunza kutokana na yaliyotokea Oktoba 29 na sasa imeongeza msisitizo katika kuimarisha weledi wa waandishi kupitia mifumo rasmi ya mafunzo.
Aidha amesema kuwa Bodi ya Ithibati ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria imekusudiwa kuwa nguzo ya kulinda, kukuza na kuimarisha ubora na weledi wa wanahabari nchini ikiwemo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uhuru lakini kwa kuzingatia maadili na usalama.
Mhe. Prof. Kabudi alisema tukio la Oktoba 29 lilikuwa la kipekee na halijawahi kutokea nchini na limeonesha Serikali kuwa bado hakuna waandishi waliotabahali katika maeneo nyeti kama uandishi wa migogoro machafuko usalama na masuala ya kiulinzi.
Alisisitiza pia umuhimu wa waandishi wa habari kutabahali yaani kubobea katika eneo maalumu la uandishi kulingana na aina ya taarifa wanazoripoti.
“Kwa yaliyotokea Oktoba 29 ni wazi kwamba hata usalama wa waandishi wa habari ulikuwa hatarini.
Hivyo mafunzo ya namna ya kuripoti katika mazingira hatarishi ni lazima yawe sehemu ya utaalamu watakaoupata kupitia Bodi ya Ithibati,” alisema.
Amesisitiza kuwa uandishi wa habari unahitaji utaalamu maalumu kulingana na eneo husika hivyo si kila mwandishi anaweza kuripoti kila tukio Kwa mfano alisema waandishi wanaotumwa kuripoti maeneo yenye migogoro nje ya nchi hupatiwa mafunzo ya kisaikolojia mbinu za kujilinda matumizi ya vifaa vya kujihami kama bulletproof pamoja na miongozo ya namna ya kuandika taarifa bila kuhatarisha usalama wao .
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime