Mwanza yazindua utoaji elimu ya bima ya afya kwa wote

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, leo Desemba 17 mwaka huu amezindua utoaji wa elimu ya Bima ya Afya kwa Wote mkoani Mwanza, akihimiza wananchi kushiriki ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu.

Mhe. Mtanda amesema bima ya afya huwezesha wale wachache wanaougua kupata matibabu kwa urahisi, kwani si wote wanaochangia huugua kwa wakati mmoja. 

Amewataka viongozi na wataalamu kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha wananchi, akisisitiza kuwa bima ya afya ni jambo la msingi lenye faida kubwa kwa jamii.

Aidha, amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wataalamu wanapatiwa elimu na semina za kutosha ili kuongeza uelewa kuanzia ngazi ya juu hadi jamii. 

Pia amewataka watoa huduma za afya kuboresha huduma kwa wateja ili wananchi waone fahari ya mfumo huo, akisisitiza uwajibikaji na uongozi bora katika utoaji wa huduma.

Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa amebainisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya afya mkoani humo, akisisitiza kuwa maendeleo hayo hayatakuwa na maana iwapo wananchi hawatapata huduma, ndiyo maana matumizi ya bima ya afya yanahamasishwa.

Kwa upande wake, Dkt. Carolyne Damiani Mkurugenzi Msaidizi Uratibu Bima ya Afya kutoka wizara ya Afya ameeleza dhana ya bima ya afya ikijumuisha malipo kabla ya huduma, uchangiaji wa pamoja, kuchangiana kati ya wenye uwezo na wasio na uwezo, usawa katika mchango na huduma, upatikanaji wa huduma bora kwa wakati, pamoja na uwajibikaji wa pamoja kati ya Serikali, skimu za bima, vituo vya afya na wananchi.

Utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya mwaka 2023 iliyopitishwa na Bunge, Ilani ya Uchaguzi ya 2020, Dira ya Taifa 20250 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii