Msako wa Kuwakamata Kamchape waanza rasmi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewataka wananchi kuachana na imani potofu ikiwemo kuamini katika ushirikina ambao unaweza kuchochea mauaji, ukatili na matukio mengine ya jinai katika baadhi ya maeneo, hususan katika Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Kauli hiyo imetolewa Disemba 17 mwaka huu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, alipofanya mkutano wa hadhara na wakazi wa Kata ya Bwisya wilayani humo kwa lengo la kutoa elimu ya usalama na kuhimiza utunzaji wa amani.  

Akizungumza kwenye mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa Serikali, dini na wananchi, DCP Mutafungwa amesema jukumu la kudumisha amani ni la kila mmoja, hivyo kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu wanaojiita wataalam wa kusaka wachawi maarufu kama ‘Kamchape’.

Amebainisha kuwa kundi hilo limekuwa likijihusisha na uporaji wa mali, utapeli kwa kutumia ramli chonganishi na kuingia katika nyumba za watu kwa madai ya kuondoa ushirikina jambo ambalo linajenga chuki na kukiuka sheria za nchi.

“Hatutaruhusu watu binafsi au viongozi kuwatapeli wananchi kwa kisingizio cha matambiko au imani za kishirikina. Jeshi la Polisi liko tayari kulinda raia na mali zao wakati wote,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha kuwahifadhi wahalifu hao (Kamchape)badala yake watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa sheria.  

Aidha, Kamanda Mutafungwa amesema watu 21 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na vitendo hivyo vya kihalifu na uchunguzi dhidi yao unaendelea, utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kisiwa cha Ukara, akiwemo Maritha Nyangeta na Samsoni Ibrahim, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufika kisiwani hapo na kutoa elimu, wakisema hatua hiyo imewaondolea hofu waliyoishi nayo kwa zaidi ya miezi mitatu.  

Wamesema wamekuwa wakilengwa na kundi la Kamchape linalopita nyumba kwa nyumba, kuwatisha na kuwanyang’anya mali zao kwa madai ya kuwatoa uchawi, hali iliyozua taharuki na kuathiri maisha yao ya kila siku.

Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na msako mkali dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo hadi pale vitakapotokomezwa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii