Mwigulu atoa taarifa hali ya ukame nchini, ahimiza kutunza chakula

Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ametoa taarifa kuhusu hali ya ukame nchini, huku akiwataka Watanzania kutunza na kutumia kwa uangalifu akiba ya chakula waliyonayo kutokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua.

Wito huo umetolewa Desemba 14, mwaka huu, wakati Waziri Mkuu alipokutana na baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutoka mikoa ya Dodoma na Singida, katika ofisi zake Mlimwa, jijini Dodoma.

Alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, pamoja na mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili 2026. Kwa mujibu wa utabiri huo, baadhi ya maeneo nchini yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, huku yakikabiliwa na vipindi virefu vya ukame na mtawanyiko usioridhisha wa mvua.

“Kwa kuzingatia utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kukumbwa na mvua chache, hali itakayodumisha vipindi virefu vya ukavu,” alisema.

Alieleza kuwa tathmini ya TMA inaonesha uwezekano wa kuchelewa kwa msimu wa mvua katika mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa kwa sasa hakuna tishio la uhaba wa chakula nchini kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo. Pamoja na hali hiyo, amewasihi wananchi kuendelea kutumia chakula kwa uangalifu na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.

“Ingawa tuna akiba ya chakula ya kutosha, ni muhimu wananchi wakaendelea kuweka akiba na kutumia chakula kwa nidhamu,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliwakumbusha wakulima kuandaa mashamba yao kwa wakati na kutumia pembejeo zinazofaa kulingana na upatikanaji wa mvua chache. Pia amewahimiza kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ambao kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

Dk. Mwigulu pia aliwataka wafugaji kuweka mipango madhubuti ya matumizi na uhifadhi wa maji pamoja na chakula cha mifugo ili kukabiliana na athari za hali ya ukame.

Vilevile, aliwasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha maafisa ugani wanawatembelea wakulima mara kwa mara mashambani na kutoa ushauri wa kitaalamu, ikiwemo matumizi sahihi ya mbegu kulingana na hali ya hewa, badala ya kukaa ofisini kwa muda mrefu.

“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri endeleeni kuhamasisha wakulima wajisajili kwenye daftari la mkulima na kuhakikisha wanapata namba za usajili,” alisisitiza.

Aidha, alizitaka taasisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuhakikisha shehena za pembejeo zinahudumiwa kwa wakati bandarini ili kusambazwa kwa ufanisi kwa wakulima nchini.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii