M23 yawataka raia wa DRC waliokimbia warejee nchini mwao

Msemaji wa AFC/M23 Lawrence Kanyuka amewataka wakongomani kurejea nyumbani akitaja kuwa kwa sasa hali ya usalama ni shwari.

Msemaji wa kundi hilo linaloungwa mkono na Rwanda amesema: "Kila kitu kinaendelea vizuri huko Uvira hivyo wanatoa wito kwa raia wenzeo ambao bado wako nje ya nchi kama  Burundi na maeneo mengine waweze kurudi nyumbani kwani maisha yamerejea kama kawaida na usalama unahakikishwa na AFC/M23."

Pia M23 imesema mamia ya  askari wa Burundi  wamekamatwa katika mapigano ya hivi majuzi huko Kivu Kusini na kuwa kwa sasa wako salama na watarejeshwa nchini mwao ikiwa serikali ya Burundi itafanya ombi la kuwarejesha kwa kufuata sheria za kimataifa.

Aidha mapigano yameendelea katika baadhi ya maeneo licha ya onyo la Marekani iliyoitupia lawama serikali ya Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya Washington Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema watachukua hatua ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwa rais Donald Trump zinatimizwa.

Hata hivyo  Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limetahadharisha kuwa kitendo cha mji wa Uvira kuangukia mikononi mwa waasi wa M23 kunahatarisha usalama wa wananchi wa eneo hilo na kuwataka wadau wote kuwezesha raia wanaokimbia mapigano kuondoka salama na kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inawafikia wale wote wenye uhitaji.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii