Rais Alexander Lukashenko wa Belarus ametowa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha vita nchini Ukraine wakati huu Marekani ikiendelea na juhudi za kidiplomasia kuhusu mzozo huo uliodumu kwa miaka minne sasa.
Kupitia mahojiano yaliyochapishwa siku ya Jumanne Disemba 16 mwaka huu mshirika huyo muhimu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi amemsifia na kumuunga mkono Rais Donald Trump wa Marekani akidai kuwa lau angelikuwapo tangu awali vita hivyo kamwe visingetokea.
Lukashenko ambaye aliruhusu nchi yake kutumiwa na Urusi kuivamia Ukraine mwaka 2022 amesema Trump ndiye anayetegemewa sasa kusitisha vita hivyo na kwamba anahitaji kutiwa moyo.
Kauli ya Lukashenko imetolewa ikiwa ni siku moja tu baada ya mkutano wa pande tatu uliofanyika mjini Berlin, Ujerumani, ambapo wawakilishi wa Marekani, Ulaya na Ukraine walisema wamepiga hatua kubwa kuelekea makubaliano ya kukomesha vita hivyo kupitia mpango wa amani uliopendekezwa na Trump.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime