MIILI mitano kati ya 33 iliyofukuliwa katika kaburi la pamoja Makaburini mjini Kericho ina majeraha kichwani yaliyosababishwa na kupigwa kwa vitu butu, hali iliyozua maswali mapya kuhusu vifo hivyo vya kutatanisha.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, jumla ya miili 33 wanaume watu wazima wanane na watoto 25 ilifukuliwa pamoja na viungo sita vya binadamu vilivyokuwa vimezikwa katika kaburi la pamoja.
Maafisa wa upelelezi sasa wameingia hatua ya pili ya uchunguzi ili kutambua marehemu. Hadi sasa hakuna mtu aliyejitokeza kudai miili hiyo.
Daktari Richard Njoroge, mwanapatholojia wa serikali katika kesi hiyo, alisema vifo vilitokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa hewa, nimonia kali, maambukizi makubwa, kuganda kwa damu na majeraha ya kichwani.
“Wawili walifariki kutokana na majeraha ya kichwani yaliyotokana na kupigwa kwa vitu butu, kulikosababisha kuvunjika kwa fuvu la kichwa mara kadhaa,” alisema Dkt Njoroge. Aliongeza kuwa miili minne ya watoto na mtu mmoja mzima ndiyo iliyokuwa na majeraha hayo, jambo linaloibua shaka kuhusu uwezekano wa mauaji.
Aidha, alifafanua kuwa viungo vilivyopatikana vilikuwa ni matokeo ya upasuaji wa kitabibu kutokana na magonjwa sugu, na hivyo havikuhusishwa moja kwa moja na uhalifu.
Mkurugenzi wa Idara ya Mauaji katika DCI, Martin Nyuguto, alisema uchunguzi sasa unalenga kuchunguza uwezekano wa mauaji ya kiholela na biashara haramu ya viungo vya binadamu, huku eneo la uchunguzi likihusisha kaunti za Kericho na Nyamira.
Utata umeongezeka baada ya kubainika kuwa kulikuwa na mkanganyiko katika idadi ya miili iliyozikwa. Hati mbalimbali zilionyesha miili ilikuwa 13 au 14, lakini baada ya kufukuliwa iligundulika kuwa ni 33 pamoja na viungo sita.
Ripoti ya wanapatholojia pia ilibaini kuwa baadhi ya miili ilikuwa imeoza sana huku mingine ikiwa bado mipya, ikionyesha uwezekano wa vifo kutokea nyakati tofauti. Miili ya watoto 25 ilikuwa ya wasichana 10, wavulana wanane na saba ambao haikuweza kubainishwa jinsia kutokana na kuoza.
Wanasheria wamekosoa jinsi miili hiyo ilivyoshughulikiwa, wakisema iliwekwa kwenye magunia kabla ya kusafirishwa kutoka Nyamira hadi Kericho kwa mazishi mnamo Machi 20, 2026, kinyume cha taratibu za kisheria.
Kwa mujibu wa sheria ya usajili wa vifo nchini, hakuna mwili unaopaswa kuzikwa bila kibali rasmi.
Mahakama ya Kericho tayari imeamuru kufukuliwa kwa miili hiyo ili kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi, ikiwa ni pamoja na vipimo vya DNA na sumu.
Wakati huo huo, maafisa wawili afisa wa afya ya umma wa Nyamira na mhudumu wa makaburi wanazuiliwa kwa siku 30 huku uchunguzi ukiendelea, huku maswali mengi yakisalia bila majibu kuhusu chanzo cha vifo na mazishi ya siri ya miili hiyo.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime