Wawakilishi katika mazungumzo ya Urusi na Ukraine wamekubaliana juu ya haja ya kutenga njia salama ya kupitisha misaada ya kiutu na uwezekano wa kusitisha mapigano kwa raia wanaokimbia machafuko. Hiyo ni ishara ya kwanza kuelekea uwezekano wa kupatikana mwafaka tangu uvamizi ulipoanza. Mzungumzaji mkuu wa Urusi amesema mazungumzo yao yamekuwa na maendeleo makubwa.
Lakini mwakilishi mkuu wa Ukraine amedai kwamba mazungumzo hayo hayajazaa matunda ambayo Kyiv ilikuwa ikiyatarajia, lakini pande zote mbili zimekubaliana juu ya suala la kuwahamisha raia. Pia wamekubaliana juu ya usambazaji wa madawa na vyakula katika maeneo ambako mapigano makali yanaendelea. Rais Vladmir Putin amesema operesheni za kijeshi zinaendelea kama zilivyopangwa na amewasifu askari wa nchi hiyo kuwa mashujaa. Kwa upande wake rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema yuko tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Putin.