Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza kupita njia zinazotumiwa na baadhi ya bandari kubwa duniani katika kuboresha na kuendeleza miundombinu yake ili kuongeza tija, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kimataifa.
Hatua hiyo inakuja wakati mamlaka hiyo ikiwa imetangaza kuanza kutekeleza tozo ya maendeleo ya miundombinu ya bandari (Ports Infrastructure Development Levy), mfumo unaolenga kuwezesha upatikanaji wa rasilimali za kuendeleza magati, kuongeza uwezo wa bandari, kuboresha huduma za usafirishaji wa mizigo na kuandaa miundombinu ya kukidhi mahitaji ya biashara ya miaka ijayo.
Tozo hiyo ya maendeleo ya miundombinu ya bandari, ambayo inatarajiwa kuanza kutumika Julai 1, 2026 kwa kiwango cha asilimia 4.5 ya thamani ya CIF ya shehena baada ya kupunguzwa kutoka asilimia 9 iliyokuwa imependekezwa awali, inalenga kusaidia TPA kuendelea kuimarisha miundombinu ya bandari na kuongeza uwezo wa kuhudumia biashara inayokua kwa kasi ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa bandari zinqzotumia mfumo huo wa ada na tozo kujiboresha na kuendelea kuwa vinara wa biashara ya baharini duniani ni Bandari ya Rotterdam nchini Uholanzi, Bandari ya Singapore nchini Singapore, Bandari ya Shanghai na Hong Kong nchini China, Bandari ya Los Angeles nchini Marekani, Bandari ya Hamburg nchini Ujerumani, Bandari ya Antwerp nchini Ubelgiji, Bandari ya Jebel Ali nchini Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Bandari ya Tanger Med nchini Morocco.
Bandari hizi zimekuwa zikihudumia mamilioni ya makontena na mamia ya mamilioni ya tani za mizigo kila mwaka, zikiunganisha mabara mbalimbali kupitia biashara ya mafuta, gesi, magari, bidhaa za viwandani, malighafi za uzalishaji, bidhaa za kilimo na bidhaa za matumizi ya kila siku.
Inaelezwa kuwa bandari hizo kwa miaka mingi zimekuwa zikitumia tozo na ada mbalimbali za watumiaji wa bandari kama chanzo muhimu cha fedha za kuendeleza miundombinu yake, hatua iliyoziwezesha kuendelea kupanua uwezo wa kuhudumia mizigo, kuvutia biashara zaidi na kuimarisha nafasi yake katika uchumi wa dunia.