Enzo Maresca Kurithi Kiti cha Guardiola Manchester City

Manchester City imemtangaza Enzo Maresca kuwa kocha mkuu mpya wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Pep Guardiola na kuanza rasmi enzi mpya katika kikosi hicho cha Ligi Kuu England.

Maresca, mwenye umri wa miaka 46, amesaini mkataba wa miaka mitatu kuinoa City. Taarifa za kutangazwa kwake zilichelewa kutokana na mazungumzo kati ya Manchester City na Chelsea kuhusu fidia, kufuatia kuondoka kwake katika klabu hiyo ya London mwezi Januari.

Kocha huyo raia wa Italia si mgeni ndani ya Manchester City. Aliwahi kuifundisha timu ya akademi ya klabu hiyo msimu wa 2020/21 kabla ya kuwa msaidizi wa Pep Guardiola msimu wa 2022/23.

Katika kipindi hicho, Maresca alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lililoiongoza Manchester City kutwaa mataji matatu makubwa kwa msimu mmoja, likiwemo Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA.

Sasa Maresca anakabiliwa na jukumu kubwa la kurithi mafanikio ya Guardiola, ambaye anaondoka akiwa ametambulika kama mmoja wa makocha bora zaidi katika historia ya soka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii