Kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye, ilianza siku ya Jumanne jijini Kampala wakati huu, wanaharakati na wapinzani wa rais Yoweri Museveni wakiendelea kukamatwa akiwemo Miria Matembe ambaye amefunguliwa mashtaka ya uchochezi na kuzuiwa kwenye gereza la Luzira.
Besigye amekataa kuendelea kwa kesi yake, hadi pale Mawakili wake watakapohakikishiwa usalama wao. Mmoja wa Mawakili wake kutoka nchini Kenya Martha Karua alifukuzwa nchini Uganda wiki iliyopita.
Besigye alikuwa na kauli hii mbele ya Mahakama.
‘‘Mawakili wetu wamejificha na sasa wanatuambia tuwatafute wengine ambao hawatajificha.Hii ni ngumu sana kwa sababu mtu anayewahangaisha ndiye mshtakiwa.’’ Alisema Besigye.
Katika hatua nyingine, Waziri wa mawasiliano wa Uganda, Justine Lumumba Kasule, amesema kufungiwa kwa vyombo vya Habari vya kampuni ya NMG kumetokana na uchunguzi unaoendelea ambao uliagizwa na rais Yoweri Museveni dhidi ya taasisi hiyo.
‘‘Matukio ya tarehe 28 Juni mwaka huu, yaliosababisha kufungwa kwa kampuni ya NMG yalisababishwa na uchunguzi wa kiusalama ulioanzishwa na Rais Museveni.’’ Alisema Justine Lumumba Kasule.