Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff, ameipongeza Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO) pamoja na taasisi nyingine zilizoshinda Tuzo za East Africa Public Service Awards 2026 kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuchangia maendeleo ya uchumi wa mataifa yao.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Juni 30, 2026, jijini Dar es Salaam, Mhe. Shariff amesema tuzo hizo zinatoa motisha kwa taasisi mbalimbali kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.
Kwa upande wake, Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala ETDCO, Bw. Thomas Mwinuka, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa juhudi na kujituma kwao katika kuhakikisha wanatekeleza malengo ya kampuni kwa ufanisi.
“Tuzo hii ni ishara ya kutambua juhudi na mchango wa wafanyakazi wa ETDCO. Itatuongezea ari ya kufanya kazi kwa uwajibikaji zaidi, tutaendelea kutoa huduma bora kwa kuwa maendeleo endelevu ya sekta ya miundombinu ya umeme kwani ni msingi muhimu wa ukuaji wa nchi yetu na ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Bw. Mwinuka.
Aidha, amewapongeza waandaaji wa Tuzo za East Africa Public Service Awards kwa kutambua na kuthamini mchango wa ETDCO katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Katika tuzo hizo, ETDCO imeibuka mshindi wa jumla wa Tuzo ya Ubora Afrika Mashariki katika Maendeleo ya Miundombinu ya Umeme kwa mwaka 2026, iliyotolewa na East Africa Public Service Awards.