Katibu Mkuu wa Chama cha Frelimo cha nchini Msumbiji Chakil Aboobakar amesema ni muhimu kwa vyama sita vya ukombozi Kusini mwa Afrika kuendelea kushikamana na wananchi hususani katika mapambano dhidi ya uchumi yatakayowaondoa kwenye utegemezi.
Amesema vyama hivyo vinatakiwa kutumia maarifa wanayoyapata kuhakikisha vinatanguliza maslahi ya wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.
Chakil ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo kwa wakufunzi 37 kutoka vyama vitano vya ukombozi kusini mwa Afrika yaliyokuwa yakifanyika katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha.
Pia amesema njia hizo ni muhimu kuzingatiwa kwakuwa wapo maadui wa zamani ambao wamebadili mbinu kwasasa wakionyesha ni marafiki wa karibu na nchi zao na kuonekana kutaka kuwasaidia na kuwaunga mkono kwenye vitu mbalimbali.
"Hatupaswi kuwaruhusu watu wanaotuchukia kutumia changamoto zetu kutugawa, badala yake tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na kwa umoja ili kutatua changamoto zetu," amesema
Ameongeza kuwa nchi hizo zina jukumu la kuwaandaa vijana kufanya kazi kwakuwa ipo idadi kubwa ya kundi hilo halina ajira linaishi katika hali ya uhitaji na ni kazi pekee ya kuwaweka kwenye uhuru wa kujitegemea.
Kadhalika amewakumbusha wakufunzi hao kujikita kubuni mbinu za kukwamua vyama vyao kwenye umasikini kuwapa njia ya kukua kiuchumi kuendana na hali ya sasa.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Agrey Mwanri, amewataka wawakikishi hao wa chama kuendelea kubaki na dhamira yao ya kuungana na wananchi na kuimarisha umoja kwenye vyama vyao.
Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Prof. Marselina Chijoriga amesema walikuwa na kundi zuri la wataalamu waliowafundisha wahitimu hao wakiwemo mawaziri wa zamani, makatibu wakuu wa zamani, maprofesa na wahadhiri wenye sifa za juu.
Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ufungwaji wa mafunzo hayo yamefanyika kwa vyama vitano kati ya sita vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, washiriki wakiwa 37 kati yao kumi ni CCM.
Prof. Ole Gabriel amesema wamewasisitiza wakufuzi hao kutoka vyama sita rafiki wafikirie namna ya kupata uhuru wa kiuchumi kuondokana na utumwa kwenye nchi zao.
Kati ya vitu walivyofundishwa kwenye mafunzo hayo ni pamoja na utawala bora, mawasiliano ya kimkakati, maadili, fikra za kisiasa na maandalizi ya wale wanaokuja kuchukua majukumu ya uongozi, uhuru wa kiuchumi na masuala ya kisiasa.
Hafla hiyo ya kufunga mafunzo yaliyodumu kwa siku 45 ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani, Mizengo Pinda, wajumbe kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), mabalozi na makamishna wakuu, watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu, wasomi na wawakilishi wa mashirika ya kibiashara.