Mwanamke aliyefungwa miaka 10 jela kwa kukutwa na kilo 26.9 za bangi chini ya kitanda, ameachiwa huru baada ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mwanza, kubaini upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.
Mshtakiwa huyo Anita Marwa, aliachiwa huru jana mbele ya Jaji Mfawidhi Sedekia Kisanya, baada ya kusikiliza rufani iliyowasilisha akipinga hatia ya adhabu aliyopewa na Mahakama ya Wilaya ya Ngamagana, Mwanza, Juni 18,2026.
Awali, Anita alishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume na Kifungu cha 16(1) na (2) cha Sheria ya Udhibiti na Utekelezaji wa Dawa za Kulevya, Sura ya 95, Toleo la 2023.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa, Oktoba 27, 2025, katika eneo la Kishiri ‘A’, Wilaya ya Nyamagana, Jiji na Mkoa wa Mwanza, Anita alikutwa akimiliki kinyume cha sheria bangi yenye uzito wa kilogramu 26.9.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliita mashahidi saba na kuwasilisha vielelezo mbalimbali na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wawili.
Upande wa Jamhuri katika ushahidi wao, ilidaiwa dawa hizo zilipatikana chini ya kitanda cha mshtakiwa pamoja na mifuko 29 yenye rangi nyekundu isiyo na kitu, pochi, simu mbili za Tecno, simu moja ya Samsung na fedha tasilimu, Sh 79,000.
Mtaalamu kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Amani Samwel, alidai alipozifanyia uchunguzi dawa hizo, alibaini kuwa ni bangi kilogramu 26.9.
Mshtakiwa katika utetezi wake, pamoja na shahidi mmoja wa upande wake, walikanusha tuhuma hizo na kudai bangi hazikukutwa nyumbani kwa mshtakiwa na kwamba aliziona mahakamani.
Baada ya usikilizwaji wa shauri hilo, Mahakama ya Wilaya Nyamagana ilimtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha miaka 10 jela.
Anita hakuridhishwa na uamuzi huo aliwasilisha rufani akidai alihukumiwa kimakosa kwani mashtaka dhidi yake hayakuthibishwa na upande wa mashtaka.
Mrufani aliwakilishwa na Wakili, Mussa Malongosi na wajibu rufani, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benedict Kapela na Wakili wa Serikali, John Komba.
Mahakama Kuu baada ya kupitia ushahidi, ilibaini kuwa ushahidi wa mtaalamu kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ulikuwa na tatizo kwani vitu alivyopokea kwa ajili ya uchunguzi vilikuwa na nyasi zilizokauka zilizochanganyika na mbegu.
Jaji Kisanya alisema suala hilo lilikuwa muhimu kwa sababu Sheria ya Udhibiti na Utekelezaji wa Dawa za Kulevya inatofautisha bangi na mbegu za mmea wa bangi.
"Mtaalamu hakueleza ni kiasi gani cha kilo 26.9 kilikuwa nyasi za bangi na ni kiasi gani kilikuwa mbegu. haikuwezekana kubaini kama uzito wote wa kilogramu 26.9 uliotajwa katika shtaka ulikuwa bangi inayotambuliwa na sheria.
"Mahakama ilibaini kutokuwapo kwa ulinganifu katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka. Mashahidi waliodai kushuhudia ukamataji, uhifadhi na ufungaji wa vielelezo walieleza kuwa vilikuwa nyasi zilizokauka, lakini mtaalamu wa maabara ndiye aliyesema vilikuwa nyasi zilizokauka zilizochanganyika na mbegu.
"Kwa maoni ya mahakama, tofauti hiyo haikuwa ndogo kwa kuwa ilihusu utambulisho na muundo wa kitu kilichokuwa msingi wa shtaka.
"Tofauti kati ya ushahidi wa mtaalamu wa maabara na mashahidi wengine ilizua shaka kuhusu iwapo kitu kilichofanyiwa uchunguzi na mtaalamu huyo ndicho kilekile kilichodaiwa kukamatwa nyumbani kwa Anita.
"Upande wa mashtaka ulipaswa kuthibitisha bila kuacha shaka ya msingi, kwamba kitu kilichodaiwa kukutwa kwa Anita kilikuwa bangi na kwamba kilikuwa na uzito wa kilogramu 26.9,"alisema Jaji Kisanya.
Mahakama ilihitimisha kuwa, kulikuwa na shaka ambayo haikuweza kuondolewa kuhusu muundo na uzito wa dawa hiyo, pamoja na kushindwa kuthibitisha mlolongo usiokatika wa utunzaji wa vielelezo.
Kutokana na uamuzi huo, Mahakama Kuu ilikubali rufaa, ikaifuta hukumu ya hatia dhidi ya Anita, iliondoa kifungo cha miaka 10 pamoja na amri ya kutaifisha mali iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana.
Pia mahakama hiyo iliamuru Anita Marwa aachiliwe mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.