Watu 12 wafariki katika ajali ya boti

Watu 12 wamethibitishwa kupoteza maisha, baada ya boti waliyokuwa wanasafiria kuzama kwenye Ziwa Kivu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Jumapili, baada ya boti hiyo kuanza safari kutoka Bukavu, ikielekea kaika kisiwa cha Idjwi huko Kivu Kusini.

Mpaka sasa, abiria kadhaa, hawajawapatikana, huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.

Boti hiyo iliyotengezwa kwa mbao, ilikuwa inawasafirisha wafanyabiashara wadogowadogo waliokuwa wametokea katika kisiwa cha Idjwi na walikuwa wanarejea nyumbani, kutoka Bukavu na bidhaa mbalimbali walizokuwa wamenunua.

Omar Akilimali, mmoja wa waokoaji amesema, boti hiyo ilionekana kulemewa na uzito wa abiria na mizigo kabla ya kuzama. Aidha, Akilimali ameemeleza kuwa, watu 15 wameokolewa. Taarifa zinasema, abiria zaidi ya 50 walikuwa ndani ya boti hiyo.

Usafiri wa majini wenye hatari ndio njia pekee kwa wakaazi wa kisiwa cha Idjwi kufika katika maeneo mbalimbali ukiwemo mji wa Bukavu, wengine wakienda sokoni na hata shule kwa wanafunzi.

Ajali kama hizi hufanyika mara kwa mara kwa sababu ya hali mbaya ya boti, abiria kupita kiasia na ukosefu wa vifaa vya kujiokoa janga kama hili linapotokea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii