Akamatwa Kwa Tuhuma za Kuwatupa Watoto Wake Kutoka Ghorofa ya Sita

Mwanaume mwenye umri wa miaka 25 amekamatwa nchini Japan kwa tuhuma za kujaribu kuwaua watoto wake wawili, baada ya kudaiwa kuwatupa kutoka kwenye roshani ya ghorofa ya sita ya jengo la makazi.

Tukio hilo lilitokea mapema Jumamosi, Septemba 26, katika mji wa Kakamigahara, mkoani Gifu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Japan, mtuhumiwa huyo, Tomokazu Miura, alidaiwa kuwatupa watoto wake wawili, msichana mwenye umri wa mwaka mmoja na mwingine mwenye umri wa miaka minne, kutoka kwenye roshani ya nyumba yao.

Watoto hao walianguka kutoka urefu wa takribani ghorofa sita, lakini waliangukia kwenye mikeka iliyokuwa imeandaliwa chini na wahudumu wa dharura.

Wote wawili walinusurika na kupelekwa hospitalini. Ripoti zinasema walikuwa na fahamu wakati wakisafirishwa kwenda hospitali, huku majeraha yao yakielezwa kuwa hayakuwa ya kuhatarisha maisha.

Tukio hilo lilitokea saa 4:20 asubuhi, saa za Japan, muda mfupi baada ya polisi kufika katika nyumba hiyo kufuatia simu ya dharura iliyopigwa na mke wa mtuhumiwa usiku wa kuamkia tukio.

Majira ya saa 11:30 jioni siku ya Ijumaa, Septemba 25, mke huyo aliwapigia polisi na kuwaeleza kuwa mume wake alikuwa amemshika mkono wakati wa mabishano.

Polisi walifika katika eneo hilo na kuzungumza na mwanamke huyo nje ya nyumba. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti, Miura alikataa kushirikiana na polisi na kujifungia ndani ya nyumba.

Inadaiwa kuwa wakati polisi walipokuwa wakijiandaa kuingia ndani, ndipo watoto hao walipotupwa kutoka kwenye roshani.

Kamera za usalama zilizokuwa karibu na eneo hilo zilinasa tukio hilo, huku picha zikionyesha vitu viwili visivyoeleweka vizuri vikianguka kutoka juu ya jengo.

Baada ya tukio hilo, Miura alikamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua. Vyombo vya habari nchini Japan vimeripoti kuwa alibaki kimya wakati akihojiwa na polisi.

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyedai kushuhudia polisi wakimchukua mtuhumiwa alisema kuwa Miura alidaiwa kusema kwamba alikuwa na nia ya kufa pamoja na watoto hao.

Hata hivyo, kauli hiyo ni madai ya shahidi yaliyoripotiwa na chombo cha habari na haijathibitishwa rasmi na polisi.

Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku watoto hao wakiendelea kupata matibabu hospitalini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii