Mazishi ya mwanachama wa upinzani aliyeuawa wakati wa maandamano ya C64 yazuiwa Kinshasa

Mazishi ya Manassé Lomboto, mwanaharakati wa upinzani aliyefariki kutokana na majeraha aliyoyapata waati wa maandamano ya upinzani ya Septemba 15 dhidi ya marekebisho yoyote ya katiba nchini DRC, yalizuiwa Jumamosi, Septemba 26, 2026, huko Kinshasa. Familia yake na jukwaa la C64 walipokuwa wakijiandaa kupeleka mwili wake makaburini, mamlaka ziliamuru ubaki katika chumba cha kuhifadhia maiti, kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa wa mahakama.

Mazishi ya Manassé Lomboto, mwanaharakati wa upinzani na mwanachama wa ADD Congo na jukwaa la C64, yalisitishwa, na kusababisha mvutano mkubwa siku ya Jumamosi, Septemba 26, katika Hospitali ya Cinquantenaire huko Kinshasa. Mahakama iliamuru kuahirishwa kwa mazishi hayo huku uchunguzi ukiendelea. Uamuzi huu ulisababisha hasira na kutoelewana miongoni mwa wanaharakati na familia waliokuja kutoa heshima zao za mwisho.

"Tumekuja kuchukua mwili wa Manase na kuupeleka kwenye makazi yake ya milele... Lakini tumepokea barua ikituambia hatuwezi kuupata mwili wa Manassé," alisema Prince Epenge katika video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii. Kulingana na mwanaharakati huyo, mamlaka iliwatuma maafisa wa polisi ambao walizuia chumba cha kuhifadhia maiti. "Mlango umezuiwa, na ukijitambulisha kama mwanachama wa Lamuka, C64, au ADDCongo, unafukuzwa. "Hii haijawahi kutokea! Hizi ni tabia za serikali zilizopita ambazo tulipigana nazo ambazo sasa wanazirejelea tena," aliendelea kusema mpinzani huyo. Kulingana naye, mwendesha mashtaka ambaye alituma amri ya kuzuia mwili wa Manassé hakumjulisha mtu yeyote: wala sisi, wala familia ya asili. Ni leo tu ndipo kwa ghafla anajitokeza na kusema anazuia mwili wa Manassé.

Juhudi zetu zote za kupata jibu kutoka kwa polisi hazijafanikiwa.

Kufuatia maandamano yaliyoandaliwa mnamo Septemba 15, jukwaa la upinzani C64 lilishutumu Force du Progrès, chama kilicho karibu na UDPS, kwa kushambulia wanaharakati wake huko Kinshasa na kusababisha kifo cha Manassé Lomboto. Shutuma hizi zilikanushwa na UDPS.

Kwa upande wake, Waziri wa Sheria alitangaza kuanzishwa kwa uchunguzi ili kubaini kuhusika unaowezekana katika ghasia zilizozuka wakati wa maandamano haya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii