Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, pamoja na uchaguzi wa madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume hiyo leo, Septemba 25, 2026, nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Chamwino imekuwa wazi baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Deogratias John Ndejembi, kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uteuzi wake ulifanyika tarehe 26 Agosti 2026 na kuthibitishwa na Bunge tarehe 28 Agosti 2026.
Aidha, Tume imesema imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara. Nafasi hizo zilitokana na madiwani wanane (08) kuondoka madarakani kwa nyakati tofauti na madiwani watatu (03) kujizulu.
Kata 11 zitakazofanya uchaguzi
Ratiba ya Uchaguzi
Tume imetangaza kuwa fomu za uteuzi kwa wagombea wa Ubunge Jimbo la Chamwino na udiwani katika kata hizo 11 zitatolewa kuanzia Oktoba 7 hadi Oktoba 13, 2026.
Uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe Oktoba 13, 2026.
Baada ya hapo, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe Oktoba 14, 2026 na kuendelea hadi Novemba 3, 2026.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Chamwino pamoja na uchaguzi wa madiwani katika kata hizo 11 utafanyika Jumatano, Novemba 4, 2026.
Tume imewataka wagombea, vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo ya Tume katika kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.